Manchester City yapata ushindi wa tabu dhidi ya Luton Town
12 Desemba 2023Mabao mawili ndani ya dakika tatu kipindi cha pili yaliyotiwa kambani na Bernardo Silva na Jack Grealish yaliwapa vijana wa Pep Guardiola ushindi wa tabu na kufufua matumaini ya kutetea taji lao.
Manchester City ilikuwa inaongoza jedwali la Ligi Kuu ya Premia mnamo Novemba 4 walipoifunga Bournemouth mabao 6-1 kabla ya kutoka sare michezo mitatu mfululizo na hatimaye kufungwa katikati ya wiki na Aston Villa.
Soma pia: Guardiola: Arsenal ya msimu huu ni kitisho
Mshambuliaji Erling Haaland alikosa mechi hiyo baada ya kupata jeraha katikati ya wiki na kukosekana kwake kuliikosesha uwiano klabu hiyo licha ya kudhibiti mpira kwa muda mrefu.
Na katika uwanja wa Villa Park, wenyeji Aston Villa wamechupa hadi katika nafasi ya tatu baada ya kupata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya washika bunduki Arsenal.
Aston Villa yaweka rekodi ya kushinda mechi 15 mfululizo ugani Villa Park
Bao la kipekee la Aston Villa lilitiwa wavuni na nahodha John McGinn na kuwang'oa kileleni Arsenal ambayo sasa inashikilia nafasi ya pili ikiwa na alama 36, nyuma ya Liverpool iliyopata ushindi wa 2-1 mbele ya Crystal Palace.
Kocha wa Aston Villa Unai Emery ametahadharisha kuwa msimu bado ni mchanga mno kufikiria juu ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya Premia. Ameeleza, "Nitazungumza katika mechi ya mzunguko wa 30, 32 na kama bado tutakuwepo katika nafasi za juu. Tukifika huko basi tunaweza kuzungumzia kuhusu ubingwa."
Soma pia: Erik ten Hag ajilaumu kwa sare dhidi ya Galatasaray
Washika bunduki walifunga bao la kusawazisha dakika za mwisho mwisho za mchezo lakini lilifutwa baada ya muamuzi wa kati kueleza kuwa, Kai Havertz aliunawa mpira.
Mkufunzi wa Arsenal Mikel Arteta ameonyesha kutoridishwa na uamuzi wa refarii kulifuta bao la Havertz, "Tumesikitishwa na matokeo, hasa kwa jinsi tulivyocheza. Nadhani tulistahili zaidi maana tulikuwa timu bora. Sijaona timu ikicheza vizuri msimu huu dhidi ya Aston Villa kama tulivyofanya sisi. Tulistahili kupata angalau ushindi kutokana na nafasi za wazi tulizozibuni katika mchezo."
Vijana wa Mikel Arteta sasa watalekeza nguvu zao katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mnamo siku ya Jumanne ambapo wamepangwa kuchuana na PSV Eindhoven ya Uholanzi katika mechi ya mwisho ya kundi B.