1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya abiria wanaoelekea Dubai wakwama Uganda

29 Desemba 2021

Hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupiga marufuku safari za ndege za abiria kutoka mataifa ya mashariki mwa Afrika imewaacha mamia ya abiria katika mashaka makubwa. Mamia ya abiria wamekwama Kampala

https://p.dw.com/p/44xMB
Uganda Entebbe | Entebbe International Airport
Picha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupiga marufuku safari za ndege za abiria kutoka mataifa ya mashariki mwa Afrika imewaacha mamia ya abiria katika mashaka makubwa. Miongoni mwa walioathirika ni wafanyabiashara ambao husafiri kwenda au kupitia Dubai kuelekea mataifa mengine. Aidha, idadi kubwa ya watu wanaokwenda kufanya kazi za vibarua katika nchi hizo nao wameshuhudiwa wakiwa wamekwama.

Kulingana na taarifa ya mamlaka za Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE tarehe 21 mwezi huu, walionya kuwa wangedhibiti usafiri wa abiria kutoka mataifa ambayo yamekumbwa na wimbi jipya la COVID-19. Hapo jana wametimiza marufuku hiyo kwa kuzuia safari za abiria kutoka mataifa ya Uganda, Kenya, Tanzania na Zanzibar, Ghana, Angola, Guinea, Ivory Coast na Ethiopia.

Uganda Entebbe | Entebbe International Airport
Kanuni za afya zinafuatwa katika uwanja wa EntebbePicha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Mashirika ya ndege yamethibitisha kupokea taarifa hiyo na kuelezea kuwa watawasafirisha tu abiria kutoka Dubai lakini si kuelekea nchi hiyo. George Wangaya na Zakia Namono ni mawakala wa mashirika ya safari za ndege wa Entebbe.

Abiria wengi waliokuwa wamefika kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe wakijiandaa kusafiri kuelekea au kupitia Dubai ndiyo waathirika wa kwanza kuhusiana na mafuruku hiyo ambayo muda wake haujaelezwa na mamlaka za Dubai. Ni kutokana na hilo ndipo wafanyabiashara wengi pamoja na makampuni yanayowapeleka vibarua nchini humo wamejikuta mashakani.

Angalau vibarua mia mbili, wengi wao wakiwa wanawake hutokea au kupitia Uganda kila siku kwenda au kupitia Dubai kwenda kufanya kazi. Hii ina maana kuwa ndoto zao za kuingiza kipato zimesitishwa kwa muda. Mamlaka ya Uganda ya safari za ndege imewashauri abiria kuwasiliana na mashirika ya ndege ili wakubaliane jinsi watakavyoshughulikiwa. Kwingineko, vyombo vya habari nchini Uganda vimepinga agizo la serikali kurusha matangazo ya tahadhari kuhusu COVID-19 ila tu baada ya matangazo hayo kulipiwa.

Lubega Emmanuel DW Kampala