1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo si Shwari Congo-Brazzaville

20 Oktoba 2015

Utawala Jamhuri ya Kongo umeyapiga marufuku maandamano yaliyokuwa yakitegemewa kufanyika leo baada ya upinzani kuitisha hatua hiyo kumpinga rais Denis Sassou Nguesso kutaka kurefusha kipindi chake madarakani.

https://p.dw.com/p/1Gr4Z
Picha: dapd

Taarifa zinasema kiasi ya watu watatu wameuwawa kwa kupigwa risasi na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati wa maandamano hayo ya kuipinga serikali ya rais Denis Sassou Ngeso katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo.Tukio hilo limethibitsihwa pia na ripota wa shirika la habari la Reuters aliyeshuhudia miili ya waliouwawa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha mjini Brazzaville.

Kwa mujibu wa ripota huyo,shahidi mmoja aliyelepeleka miili ya watu hao katika chumba hicho cha kuhifadhi maiti alisema rafiki yake alipigwa risasi na vikosi vya usalama na binafasi alikuwepo na kushuhudia kitendo hicho.Inaelezwa kwamba mawasiliano ya simu za mkononi yalikatizwa katika mji mkuu Brazzaville kabla ya mkutano huo wa kupinga hatua ya kufanyika kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba iliyopangwa kufanyika jumapili hii.

Mabadiliko ya katiba yanadhamiria kumfungulia njia rais Sassou Nguesso kugombea kwa mara nyingine tena katika uchaguzi mwingine.Nguesso anapania kujirefushia kipindi cha kubakia madarakani baada ya kuingia madarakani kupitia uchaguzi mwaka 1997 kufuatia nchi hiyo kushuhudia kwa kipindi kifupi mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha umwagikaji damu mkubwa.

Denis Sassou Nguesso rais wa Jamhuri ya Kongo
Denis Sassou Nguesso rais wa Jamhuri ya KongoPicha: picture-alliance/dpa/A. Ammar

Mwanajeshi huyo wa zamani wa kimaxisti aliwahi kuitawala Kongo kutokea mwaka 1979 hadi 1992. Inatajwa kwamba hii leo saa chache kabla ya kutolewa tangazo la kupigwa marufuku maandamano hayo polisi walifyetua risasi hewani kuwatawanya vijana waliojitokeza kwa wingi kutia moto matairi yaliyosababisha wingu zito la moshi katika miji ya majimbo ya Kusini ya Bacongo na Makelekele.Aidha mashahidi wamearifu kwamba idadi isiyokuwa ya kawaida ya wanajeshi na polisi ilitamwagwa kupiga doria katika majimbo hayo tete ya kusini ambayo yanatajwa kuwa ngome ya upinzani.

Halikadhalika mambo yaliykuwa sio shwari katika eneo la magharibi la mji wa Brazaville.Mwandishi wa Reuters anasema kwamba huduma za mawasiliano ya internet kwa simu,ujumbe mfupi wa sms na hata matangazo ya shirika la habari la kifaransa RFI yalikatizwa.Maduka mengi yamefungwa na hata shule pamoja na huduma za umma huku pia uwanja wa Boulevard des Armee ambako viongozi wa upinzani waliwataka wafuasi wao wahudhuria mkutano mkuu wa hadhara mchana wa leo ulitelekezwa.

Pamoja na mikutano na maandamano hayo ya upinzani kuzuiwa na vyombo vya dola hakuna usafiri wa mabasi wa teksi uliopatikana mjini Brazaville wakati hali ikiwa ni hiyohiyo katika mji wa kiuchumi wa Pointe-Noire. Zoezi la kura ya maoni Jumapili linatajwa na upinzani kama mapinduzi ya katiba wakati pia Jumuiya ya kimataifa ikuzungumzia wasiwasi wake kuhusiana na mchakato huo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman