Kutana na Malkia wa Sheba
Malkia wa Sheba aliishi lini? Anaaminika aliishi zaidi ya miaka elfu tatu iliyopita.
Malkia wa Sheba anajulikana kwa lipi? Kufuatia kiu chake cha kupata maarifa, malikia huyu anasemekana alimtembelea mfalme Sulemani wa Israel aliyekuwa na hekima nyingi mjini Jerusalem. Historia iliyoandikwa inadokeza kuwa malkia huyu alimzalia mfalme Sulemani mwana wa kiume ambaye alikuja kuwa mfalme wa kwanza wa Ethiopia wa utawala wa Kisulemani.
Tunajuaje kuhusu kuishi kwake? Tukio hilo la Jerusalem lilinakiliwa katika nyaraka mbali mbali ikiwemo bibilia ya Kiyahudi, Quran ambamo Malkia huyo anaitwa Bilqis na katika kitabu cha kale cha Ethiopia kinachojulikana Kebre Negast ambamo anajulikana kwa jina Makeda. Ametajwa pia katika agano jipya la Bibilia kama malkia wa Kusini.
Kebre Negast ni nini? Kebre Negast mwanzo ilikusanywa katika karne ya kumi na nne nchini Ethiopia. Baadhi ya matukio yaliyomo katika nyaraka hizo yalitoka katika agano la kale na jipya, kutoka kwa Wamisri, Waarabu na Waethiopia. Kebre Negast inaeleza kwa undani kukutana kwa Malkia Sheba na Mfalme Sulemani. Hadithi hiyo inaeleza kuwa baada ya kumpa Makeda hekima yake, Sulemani alilala naye kwa usiku mmoja, tendo lililopelekea kuzaliwa kwa Mfalme Menelik wa kwanza, muasisi wa utawala wa Kisulemani nchini Ethiopia ambao uliendelea kutawala hadi Wakati Mfalme Haile Selassie alipoondolewa mwaka 1974.
Lakini Malkia wa Sheba alitokea wapi? Chimbuko la Malkia Sheba imekuwa ni kitendawili. Waethiopia wanaamini anatokea kwao, Wayemen pia wanadai kuwa ni wao kwani Sheba inamaanisha utawala wa Kiyemeni wa Saba. Waethiopia wanaamini kuwa kasri lake lilikuwa katika mji wa kaskazini mwa Ethiopia wa Aksum ambako mpaka sasa bado magofu ya kasri hiyo yanaweza kutembelewa.
Nani anavutiwa na Malkia wa Sheba? Kukutana kwa Malkia na Mfalme kwa ajili ya uchu wa maarifa mpaka sasa kunasalia kuwa mojawapo ya vivutio vikubwa kwa watu wengi. Watu kutoka maeneo mbali mbali duniani wanaonesha kuvutiwa kwao na Malkia huyo kwa njia mbali mbali aidha kupitia michoro, mashairi, vinyago au kupitia njia nyingine. Kutokana na kuwa hadithi yake inatokana na mapenzi, umoja na urafiki, ina mvuto mkubwa.
Mantegaftot Sileshi na Getachew Tedla Haile-Giorgis wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.
Mwandishi: Sileshi Getachew
Tafsiri: Caro Robi
Mhariri: Josephat Charo