1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malipo ya kodi ya Trump yabainishwa

Yusra Buwayhid
15 Machi 2017

Ikulu ya Marekani, imethibitisha kuwa Rais Donald Trump alilipa kodi ya dola milioni 38 ya mapato yake ya dola milioni 150 ya mwaka 2005. Ikulu hiyo pia imevikosoa vyombo vya habari kwa kuchapisha taarifa hizo.

https://p.dw.com/p/2ZBmn
Donald Trump USA
Picha: Getty Images/D.Angerer/Detail

Ikulu ya Marekani ilitoa taarifa hiyo muda mfupi baada ya mtangazaji Rachel Maddow wa kituo cha televisheni cha Marekani MSNBC kupokea taarifa za malipo ya kodi ya Rais Trump na kupanga kuzizungumzia nakala hizo katika kipindi chake cha jioni. Ikulu ya Marekani ilikasirishwa sana na hatua hiyo, lakini ilithibitisha kuwa ni taarifa sahihi bila ya kutoa taarifa yoyote ya ziada juu ya suala hilo.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa ni kinyume na sheria kuiba na kuchapisha malipo ya kodi bila ya ridhaa ya muhusika mwenyewe. Kulingana na sheria, kuchapisha malipo ya kodi bila ya ruhusa ni kosa linaloweza kumpatia mtu kifungo cha hadi miaka mitano jela pamoja na faini ya dola 5,000. Lakini Maddow amesema kuwa shirika la MSNBC limetoa taarifa hizo kwa maslahi ya umma kama inavyoainishwa katika katiba ya nchi.

Mwandishi habari wa habari za uchunguzi aliyeshinda tuzo ya Pulitzer, David Cay Johnson, amesema alipokea nyaraka hizo za malipo ya kodi ya Rais Trump zenye kurasa mbili katika kisanduku chake cha posta kutoka kwa mtu asiyejulikana. Alishiriki katika kipindi cha televisheni cha Rachel Maddow jana jioni kujadili nyaraka hizo na kujaribu kubashiri mtu aliyezituma ikiwa ni pamoja na uwezekano kwamba ni Trump mwenyewe ndiye aliyezituma"Kodi ya mapato ya Donald Trump ilikuwa ni kitu ambacho kila mwanahabari akitaka kukijua tokea alivyotangaza kugombea urais. Alikuwa ni mgombea pekee wa urais katika historia ya Marekani aliyekataa kudhihirisha malipo yake binafsi ya kodi. Na ndiyo maana ikawa kila mtu anataka kujua, " amesema, Jill Colvin ripota wa shirika la habari la Marekani la AP.

IRS-Zentrale in Washington D.C.
Makao makuu ya Huduma ya Mapato ya Ndani (IRS) mjini WashingtonPicha: picture-alliance/AP Photo/J. D. Ake

Colvin anasema kuna masuali mengi ambayo bado hayakupatiwa majibu kuhusu kadhia hiyo. Kwa mfano nani mwengine aliyetumiwa nakala hizo za malipo ya kodi ya Rais Donald Trump? Je, kutadhihirishwa pia malipo ya kodi ya miaka mengine mbali na hayo ya mwaka 2005? na suala kubwa ni nani aliyezidhihirisha taarifa hizo?

Trump alikataa kudhihirisha malipo yake ya kodi ya kila mwaka na kudai kuwa anafanyiwa ukaguzi wa mahesabu na Huduma ya Mapato ya Ndani (IRS) na kwamba ameshauriwa kutoonyesha malipo yake kwa umma. Lakini hakuna vigezo vya kisheria vinavyomzuia mtu anayefanyiwa ukaguzi kubainisha malipo yake ya kodi.

Wagombea urais pamoja na maraisa wote wa nyuma wa Marekani walikuwa wakionyesha wazi malipo yao ya kodi. Wakosoaji wanasema kitendo cha Trump kukataa kuonesha malipo yake ya kodi kinaashiria kuwa kuna kitu anajaribu kukificha.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton alimkosoa Trump kwa kutobainisha malipo yake ya kodi na Trump alimjibu kufanya hivyo ni werevu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/ap

Mhariri: Grace Patricia Kabogo