Mali yasema inavunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine
5 Agosti 2024Mali imetangaza kuwa inavunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine, kutokana na matamshi ya msemaji wa shirika la ujasusi la kijeshi la Ukraine GUR Andriy Yusov, kuhusu mapigano ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mapigano hayo yalisababisha mauaji ya wanajeshi wa Mali na wapiganaji mamluki wa kundi la Wagner mwishoni mwa mwezi Julai.Mamluki wa Wagner wakiri wapiganaji wake wameuwawa pamoja na wanajeshi wa Mali
Ingawa msemaji huyo hakuthibitisha kuhusika kwa Ukraine katika mapigano hayo, lakini katika maoni yake yaliyochapishwa kwenye tovuti ya shirika la utangazaji la umma la Suspilne mnamo Julai 29, alisema kwamba waasi wa Mali walipokea taarifa zote muhimu walizohitaji kufanya shambulio hilo dhidi ya wavamizi wa Urusi.
Katika shambulio hilo, waasi wa Kituareg wa kaskazini mwa Maliwalisema kuwa waliwaua mamluki 84 wa Wagner na wanajeshi 47 wa Mali, wakati wa mapigano makali.