Mali yakomboa Diabaly
21 Januari 2013Hayo yanaripotiwa wakati idadi ya raia wa kigeni waliyokufa katika kiwanda cha gesi cha In Amenas nchini Algeria ikitajwa kuwa ni 37. Serikali ya Ufaransa imejigamba kuwa, hatua hiyo ya kusonga mbele katika uwanja wa mapambano ni mafanikio makubwa katika jitihada zake za kuwaondoa waasi wa Mali ambao wameleta mtafaruku kwa zaidi ya miezi 10 sasa, na kulifanya eneo hilo kuwa kichaka cha mipango ya mashambulizi ya kigaidi duniani.
Katika taarifa yake, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, alisema kuingia kwa jeshi la Mali katika mji ulikuwa ukidhibitiwa na maadaui zao ni mafanikio kwa upande wa Mali na wao Ufaransa.
Diabaly, ni mji ulio kilomita 350 kaskazini mwa mji mkuu wa Mali, Bamako, limekuwa eneo la mapigano kwa wapiganaji waasi kutoka maeneo yao ya kuanzisha mapambano ya miji ya Mopti na Sevare.
Raia Mali wazungumza
Taarifa kutoka kwa wakaazi katika maeneo husika zinasema kuwa waasi walivua mavazi yao na kujichangaya na raia wa kawaida na wengine kuingia katika majumba makuu kuu ya udongo katika maeneo hayo. Kiasi ya magari 30 yenye silaha nzitonzito, yakiwa na wanajeshi 200 yaliingia katika Diabaly huku wakazi wa maeneo wakiwakaribisha kwa zulia jekundu na kupiga picha nao kwa furaha isiyo na kifani.
Mafanikio haya ya sasa yanapatikana wakati Umoja wa Ulaya ukitarajia kufanya mkutano kuhusu Mali, mjini Brussels Februari 5. Mkutano huo pia utahusisha Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kibisahara ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS
Raia wa Kigeni 37 wauwawa Nigeria
Katika tukio lingine Waziri Mkuu wa Algeria amsema raia wa kigeni 37 kutoka mataifa manane tofauti wamethibitika kuuwawa katika vuta nikuvute iliyodumu siku nne baada ya wanamgambo wa Kiislamu kuvamia kiwanda cha gesi cha In Amenas nchini humo.
Waziri Mkuu huyo Abdelmalek Sellal ametaja uraia amesema wateka nyara wanatoka mataifa ya Misri, Mali, Canada, Niger, Mauritani na Tunisia na kuongeza kuwa jeshi la Algeria limeshambulia eneo la kiwanda hicho na kuwauwa wanamgambo 32 na kuweza kukidhibiti kiwanda hicho.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef