Mali na Mashariki ya kati magazetini
14 Agosti 2013Mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati,Majukumu yanayomkabili rais mpya wa Mali na kupanda bei za vyakula nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizoshughulikiwa zaidi na wahariri wa Ujerumani hii leo.
Tuanzie lakini na mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina yanayotarajiwa kuanza hii leo.Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika:
Pande hizi mbili hazendi kwa dhati katika meza ya mazungumzo.Kwamba leo hazina budi,wakushukuriwa ni wamerekani na shinikizo lao.Na tunaweza kuashiria ikiwa shinikizo hilo halitakuwa na nguvu au serikali ya Marekani itaonyesha kuchoshwa kama ilivyodhihirika mara nyingi miaka iliyopita,basi na safari hii pia hakuna chochote kitakachotendeka.Kwasababu tangu Jerusalem mpaka Ramallah kuna wanaoamini kitakachofikiwa si makubaliano bali maamuzi.Wapalastina ndio watakaoondoka patupu bila ya shaka pande hizo mbili zikianza kupimana nguvu.Pengine kisiasa watashinda,kutokana na idadi ya wahanga na picha zao kuoneshwa kote ulimwenguni.Lakini lengo la mazungumzo linabidi liwe moja nalo ni kufikiwa ufumbuzi wa kuwepo madola mawili-na lengo hilo halina badala.Kwamba masuala yote yanayozusha mabishano yapatiwe ufumbuzi katika kipindi cha miezi tisa,kama ratiba ya mazungumzo inavyotaja,hilo na hasa kutokana na uzoefu,halitakuwa rahisi kulitekeleza.
Matumaini ya amani Mali
Mali pia ilichambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kufuatia uchaguzi wa rais uliompatia ushindi Ibrahim Boubacar Keita. Gazeti la "Straubinger Tagblatt/Landshuter" linaandika:
Jukumu lake kubwa litakuwa kuleta umoja katika nchi hiyo iliyogawika.Waasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam katika eneo la kaskazini wamerejeshwa nyuma na vikosi vya wanajeshi wa Ufaransa na nchi za Afrika-hawakuwavunja nguvu lakini.Ibrahim Boubacar Keita analazimika kuwavutia upande wake watuareg waliopigana upande wa wafuasi wa itikadi kali,na kuususia uchaguzi.Jumuia ya kimataifa ina jukumu la kumsaidia rais IBK kurejesha utulivu na amani nchini Mali.Hali hiyo iko mbali kabisa kufikiwa nchini humo.
:
Nalo gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linaandika:
Utaratibu wa amani ulioanza nchini Mali unadhaminiwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa,wakishiriki pia wanajeshi wa Ujerumani.Uchaguzi uliofana ni ngao katika mapambano dhidi ya vitisho vya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam.Makundi ya kisiasa nchini Mali yana jukumu kubwa la kuleta amani nchini humo,kusikilizana na watuareg na kupambana na rushwa.Lakini ni ishara njema kwamba uchaguzi wa Mali haujagubikwa na machafuko.Ufaransa na Umoja wa mataifa hawajawapa nafasi wataliban wa jangwani.Opereshini imeleta tija,kilichosalia hivi sasa ni kuhakikisha na nchi yenyewe pia inaendelea kuwa salama.
Na hatimaye wahariri wa magazeti wameimulika ripoti iliyotangazwa hivi karibuni kuhusu ughali wa maisha nchini Ujerumani. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:
Kile ambacho,kwa muda mrefu sasa kila mnunuzi anapokwenda dukani amekuwa akikishuhudia,kimethibitishwa.Vyakula ni ghali mno .Na hasa bei za mboga,bidhaa zinazotokana na maziwa na matunda zimezidi kuongezeka.Na hilo si jambo la kustaajabisha tukizingatia msimu wa baridi ambao mwaka huu ulikuwa mrefu zaidi,ukafuatiwa na mafuriko ya mto Donau na Elbe na kumalizikia na msimu wa joto kali kupita kiasi ulioharibu mavuno na kusababisha bei kwa hivyo kupanda.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo