Hisia mseto baada ya UNRWA kupigwa marufuku na Israel
29 Oktoba 2024Licha ya pingamizi kutoka Marekani na tahadhari za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wabunge wa Israel wamepitisha kwa kura nyingi mswada juu ya kulipiga marufuku shirika la UNRWA la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina.
Kulingana na mswada huo, asasi hiyo haitaruhusiwa kutoa huduma kwenye Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki. Nchi kadhaa ambazo ni washirika wa Israel pia zimeelezea wasiwasi juu ya hatua ya bunge la Israel.
Guterres aonya juu ya sheria ya kuzuia shughuli za shirika la UNRWA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonesha kusikitishwa kwake na hatua ya Israel.
Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA amesema ikiwa shirika la UNRWA litapigwa marufuku, madhara yake yatakuwa makubwa:
"Ikiwa hatutaweza kufanya kazi tena katika Ukanda wa Gaza, hasara haitakuwa tu kwa UNRWA kama watoaji huduma wakuu, lakini pia hatua hiyo itaathiri mifumo mingine wa Umoja wa Mataifa, ambayo inategemea sana jukwaa la UNRWA ambalo limewajibika hadi sasa. Hali inakaribia sana kuharibika kabisa katika Ukanda wa Gaza, uwezekano huo upo ila sijui ni lini hasa lakini tunakaribia sana kuyaona madhara makubwa hivi karibuni," alisema Lazzarini.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema nchi yake iko tayari kuendelea kutoa misaada kwenye Ukanda wa Gaza katika namna ambayo haitahatarisha usalama wa Israel.