Malala aizuru Pakistan chini ya ulinzi mkali
31 Machi 2018Malala Yousafzai, ambae amepata umaarufu kimataifa kama mpiganiaji wa haki ya elimu kwa wasichama, alipewa ulinzi mkali Jumamosi wakati akiutembelea mji alikozaliwa katika Bonde la Swat nchini Pakistan.
Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 20, alipigwa risasi wakati akiwa na miaka 14 ndani ya basi la shule, na baadae alisafirishwa na kupelekwa nchini Uingereza kwa matibabu. Katika ziara yake hiyo Malala alionekana kulengwa na machozi huku akibembelezwa na baba yake Ziauddin Yousafzai.
Njia zilifungwa wakati helikopta iliyomsafirisha ikitua karibu na nyumba ya wageni wa serikali ilioko kilomita moja kutoka sehemu alikozaliwa.
Alifuatana pamoja na kaka yake Atal Yousafzai na mwalimu mkuu wa shule ya wanafunzi wakiume ya Swat Cadet College, Guli Bagh.
Mjomba wake amesema Malala pia atakutana na marafiki pamoja na jamaa zake - kabla ya kurudi Uingereza Jumatatu.
Mwaka 2012 - baada ya jeshi la Pakistan kufanikiwa kuwafukuza wanamgambo wengi wa Taliban kutoka katika eneo la Swat - mtu aliyekuwa amebeba bunduki alilivamia basi la shule, na kuuliza "Nani ndiye Malala," na kumfyatulia risasi msichana anayejulikana kama mwanaharakati wa kutetea haki za wasichana kupata elimu.
Kabla ya kushambuliwa na kundi la Taliban, Malala alikuwa akiiandikia blogu Idhaa ya Urdu ya BBC bila ya kutumia jina lake halisi wakati kundi la Taliban lilipokuwa likilazimisha utumiaji wa sheria kali za Kiislam.
Wanafunzi wengine wawili pia walijeruhiwa katika shambulio ambalo watuhumiwa wengi waliashiliwa huru.
Malala alipata matibabu mjini Birmingham, ambako pia alimaliza masomo yake na, mwaka 2014, alikuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kupokea Tuzo ya Nobel ya Amani.
Kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu
Malala ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza, amekiambia kituo cha televisheni cha Pakistan Geo TV siku ya Ijumaa kwamba amepanga siku moja kurudi nyumbani na kugombea wadhifa wa waziri mkuu baada ya kukamilisha masomo yake Uingereza.
"Ni nchi yangu na nina haki sawa kama raia mwengine yeyote wa Pakistan," amesema Malala.
Alhamis, alimiminikwa na machozi wakati akitoa hotuba, akisema ilikuwa ni ndoto yake siku moja kuweza kurudi nyumbani baada ya miaka mingi.
Mitazamo mchanganyiko
Maoni ya wananchi wa Pakistan kuhusu Malala yamegawanyika, baadhi ya wahafidhina wanamshutumu kuwa ni kibaraka wa nchi za Magharibi, mwenye lengo la kuifedhehesha nchi yake.
Na ingawa Malala pia amepata sifa kubwa Pakistani kote kwa kurudi nyumbani, lakini kuna baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wanaojaribu kuharibu jitihada zake za kutetea haki za wanawake kupata elimu.Malala ameviambia vyombo vya habari Ijumaakwamba anategemea ukosoaji kutoka kwa wanamgambo, wenye mtizamo wa aina hiyo, lakini hafahamu kwanini baadhi ya Wapakistan wasomu pia wanampinga.
"Ninachotaka ni watu kuunga mkono lengo langu la kupigania elimu ana kuwafikiria watoto wa kike wa Pakistan wanaohitaji elimu," ameliambia gazeti la lugha ya Kiingereza la The News. "Msinifikirie mie. Sihitaji upendeleo wowote wala simtaki mtu yeyote kunikubali. Ninachikitaka mie ni wakubali kuwa suala la elimu bado ni tatizo."
Wanaharakati wa haki za wanawake, ikiwamo Nighat Dad, wamesema katika mkutano wao na Malala Alhamis - uliowekwa siri hadi dakika ya mwisho- ulikuwa ni muhimu sana.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap
Mhariri: Bruce Amani