1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya Yemen yatakiwa kufanya mazungumzo

17 Mei 2015

Imeelezwa mjini Riyadh Jumapili (17.05.2015) kwamba suluhisho kabambe tu litakalohusisha makundi yote nchini Yemen ndilo litakaloweza kutatua mzozo wa nchi hiyo iliokumbwa na vita.

https://p.dw.com/p/1FR4z
Rais Abed Mansoor Hadi wa Yemen (kushoto)wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)
Rais Abed Mansoor Hadi wa Yemen (kushoto)wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)Picha: Getty Images/Afp/F. Nureldine

Imeelezwa mjini Riyadh Jumapili (17.05.2015) kwamba suluhisho kabambe tu litakalohusisha makundi yote nchini Yemen ndilo litakaloweza kutatua mzozo wa nchi hiyo iliokumbwa na vita.

Ismail Ould Sheikh Ahmed ameuambia mkutano wa vyama vya kisiasa vya Yemen, makundi ya wasomi na ya kiraia katika mji mkuu huo wa Saudi Arabia kwamba "Hakuna suluhisho kwa mzozo huo bali kwa kufanya mazungumzo kabambe ambayo yatamjumuisha kila mtu."

Mwanadiplomasia huyo wa Mauritania yuko katika juhudi za kufufuwa mazungumzo ya amani ya Yemen kufuatia vita vya wiki kadhaa vilivyowaathiri mamilioni ya watu.

Ameyataka makundi yote yanayohusika nchini Yemen kushiriki katika mkutano wa siku za usoni bila ya masharti yoyote yale.

Waasi wa Kishia wa jamii ya Huthi wanapambana na vikosi tiifu kwa Rais alieko uhamishoni Saudi Arabia Abed Mansoor Hadi na wameteka maeneo makubwa ya Yemen ukiwemo mji mkuu wa Sanaa.

Waasi wataka mazungumzo Yemen

Waasi hao wanataka mazungumzo hayo yafanyike nchini Yemen na wanaususia mkutano huo wa siku tatu ambapo waandaaji wa mkutano huo wanasema unahudhuriwa na wajumbe 400 baadhi yao wakiwa wamebeba majambia na kuvalia vilemba.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo wa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed mjini Riyadh.(17.05.2015)
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo wa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed mjini Riyadh.(17.05.2015)Picha: Getty Images/Afp/F. Nureldine

Makamo wa rais wa Yemen Khaled Bahah ameliambia shirika la habari la AFP kwamba licha ya kutokuwepo kwa waasi hao katika mkutano huo anataraji watahudhuria mazungumzo ya baadae.

Amesema "Wameamuwa kutohudhuria mkutano huu, lakini hatimae watakuja."

Kuikombowa upya Yemen

Rasi Hadi ambaye ni nadra kuhutubia katika mkutano wa hadhara tokea vita vilipomlazimisha akimbilie kuishi uhamishoni nchini Saudi Arabia amerudia tena shutuma zake kwamba waasi hao wamefanya mapinduzi na kutenda dhuluma dhidi ya wananchi.

Rais Abed Mansoor Hadi wa Yemen akiwasili kwa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)
Rais Abed Mansoor Hadi wa Yemen akiwasili kwa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)Picha: Getty Images/Afp/F. Nureldine

Ameuambia mkutano huo kwamba wanajaribu kulikombowa taifa lao kutoka kwa wanamgambo wanaoungwa mkono na vikosi vya kigeni akimaanisha Iran ambayo imekanusha kuwapatia silaha waasi hao wa Huthi.

Hadi ambaye ameitisha mkutano huo kwa ushirikiano na Baraza la Ushirikiano la Ghuba la mataifa sita amesema kwa "uwezo wa Mwenyenzimungu,ushindi uko karibu....tunarudi tena Aden na Sanaa ........tunarudi kuijenga Yemen mpya ilioungana."

Washiriki wa mkutano

Waziri wa Uchukuzi Bader Ba- Salama ameliambia shirika la habari la AFP kwamba miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni pamoja na Vuguvugu la Kusini la mwamvuli wa iliokuwa Yemen Kusini ambayo ilikuwa huru hadi mwaka 1990.

Wahuthi wameungana na wapiganaji walio tiifu kwa Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh ambapo chama chake cha General People Congress viongozi wake wanashiriki mkutano huo.

Abdullatif al-Zayani Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba akiwasili kwa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)
Abdullatif al-Zayani Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba akiwasili kwa ufunguzi wa mkutano wa Riyadh. (17.05.2015)Picha: Getty Images/Afp/F. Nureldine

Saleh mwenyewe binafsi yuko chini ya vikwazo vya Marekani na Umoja wa Mataifa na kwa mujibu wa mkuu wa kamati ya maandalizi Abdulaziz al- Jaber mkutano huo hautomjadili Saleh

Ameongeza kusema kwamba miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kushughulikia uundaji wa katiba mpya ambayo itawasilishwa kwa wananchi wa Yemen na "kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo matokeo ya mkutano huo."

Balozi wa Uingereza kwa mji wa Sanaa, Edmund Fitton Brown akizungumza kwa niaba ya kundi la mabalozi 14 ameuambia mkutano huo wanataraji mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kwa mashauriano na makundi yote husika atapendekeza mkondo wa kufuatwa wa mapendekezo ya mkutano huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Amina Abubakar