1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Wapinzani wamesema mkutano ni lazima ufanyike chini ya UN

1 Novemba 2017

Licha ya Urusi kujitoa  kudhamini mkutano wa amani ili kufikia makubaliano ya kisiasa kuhusu mgogoro wa Syria, wapinzani nchini humo wameukataa mkutano huo wakisisitiza ufanyike Geneva, chini ya Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2ms0l
Russland Präsident Vladimir Putin
Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Getty Images/AFP/A. Zemlianichenko

Wakati huo huo, Waturuki wameuwekea mgomo mualiko wa Wasyria walio upande wa Wakurdi, huku  juhudi hizo za kuleta amani zikikabiliwa  na vikwazo siku ya Ijumaa.

Licha ya kushiriki  kimaamuzi katika vita vya Syria mwaka 2015 ikiwa upande wa Rais Bashar Al-Assad,  Urusi sasa inaamini itajiimarisha kutokana na anguko  la Dola la kiislamu IS, kwa kuzindua mchakato mpya wa kisiasa utakaopelekea kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miaka sita.

Damascus imesema ipo tayari kuhudhuria mkutano wa Sochi utakaofanyika Novemba 18 ambao umepanga kuangazia katiba mpya na kusema kuwa ni wakati sahihi, shukrani kwa ushindi wa jeshi la Syria na kusambaratishwa kwa ugaidi.

Lakini maafisa wa upande unaompinga Rais Assad, wameukataa mkutano huo na kusisitiza kuwa mazungumzo yoyote ya amani yanatakiwa yawe chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa, Geneva, ambako mazungumzo mengine ya amani yamefeli kuleta mafanikio ya kumaliza mgogoro huo tangu ulipozuka mwaka 2011.

Israel - Grenze zu Syrien
Wanajeshi wa ulinzi wa Israel wakiwa katika mpaka wa SyriaPicha: Getty Images/AFP/J. Marey

Mkutano huo unatajwa kuwa ni mkutano ``Kati ya serikali na serikali`` amesema Mohammad Alloush, mwanachama wa Kamati ya Juu ya majadiliano ya upinzani na Ofisa Mkuu wa kundi la waasi wa  la Jaish al- Islam.

Aloush aliiambia Reuters kuwa kamati hiyo ilishangazwa kuona imewekwa katika orodha ya makundi yaliyoalikwa katika mkutano huo na wakasema watatoa tamko pamoja na vyama vingine kueleza kuwa wanakataa mkutano huo.

Makundi yasema mkutano huo ni kukwepa mabadiliko ya kisiasa

Muungano wa makundi ya upinzani ya nchini Syria, wenye makao yake nchini  Uturuki, (SNC) umesema mkutano huo ni jaribio la kukwepa ``shinikizo la kimataifa la mabadiliko ya kisiasa`` nchini Syria.

``Muungano hautashiriki katika majadiliano yoyote na serikali nje ya Geneva au bila udhamini wa UN`` msemaji wa SNC; Ahmad Ramadan, ameliambia Reuters.

Mjumbe wa majadiliano wa Urusi, amesema kuwa makundi ya Syria yalioamua kukataa mkutano huo yanajiweka katika hatari ya kuachwa wakati mchakato  huo wa kisiasa ukiendelea mbele.

Urusi imealika makundi 33 ya Kisyria na vyama vya siasa katika kile ilichoita  ``Mkutano wa Syria katika majadiliano  ya Kitaifa``

Rais wa Urusi, Vladmir Putin, kwanza alidokeza wazo la mkutano huo mwezi uliopita na kusema kuwa anaamini Moscow na serikali ya Syria hivi punde itawadhibiti  waasi nchini humo.

Akisaidiwa na ndege za Urusi na wanamgambo wa Kishia wanaoungw amkono na Iran, Rais Assad amewadhibiti waasi  wa Syria ambao walikuwa wakipigana ili kumpindua,  na kumfanya kuwa imara kijeshi na waasi wakisema wamedhibiti maeneo ya magharibi.

Serikali ya Damascus na  washirika wake, wameyakomboa  maeneo ya kati na mashariki mwa Syria  kutoka katika mikono ya  IS katika miezi ya hivi karibuni. Wakati huo huo,  kampeni nyingine inayofanywa na vikosi vya Kidemokrasia vya Syria vinavyosaidiwa na Marekani(SDF) imewaondoa IS katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Kampeni nyingine tofauti kwa sasa zimekusanyika  katika ngome kuu za IS;  katika jimbo la Deir al-Zor mpakani mwa Iraq. Uamuzi wa Urusi wa kualika makundi ya Kikurd  yanayodhibiti kundi la SDF kwa mkutano wa Sochi, ulichochea hasira za Waturuki Jumanne.

 Serikali ya mjini Ankara ambayo inayaona Makundi makubwa ya Kikurdi ya Syria kuwa ni tishio la usalama wa nchi,  imesema haikubaliki kwamba majeshi ya Kikurdi ya YPG; yamealikwa.

Msemaji wa rais wa Uturuki, Ibrahim Kalin amesema maofisa wa Uturuki na wa Urusi, wamejadili suala hilo na kuwa amefanya mkutano wake ili kutatua shida hiyo mara moja.

 Uturuki inaona kuwa kundi la YPG na washirika wake wa kisiasa, PYD; ni kama tawi la kundi la chama cha wafanyakati vya Kikurdi, ambalo limekuwa likiendeleza vurugu kwa miongo mitatu nchini Uturuki.

Mwandishi: Florence Majani

Mhariri: Iddi Ssessanga