Makundi ya magaidi wa Kinazi yapigwe marufuku - Wahariri
16 Novemba 2011Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine anasema ni jambo la lazima kukipiga marufuku chama hicho cha NDP. Lakini mhariri huyo anasema lipo tatizo moja la msingi. Anaeleza kuwa anaekusudia kuchukua hatua hiyo kwa kuwatumia makachero maalumu hatafua dafu. Mhariri anaeleza kuwa pana ushahidi unaonyesha kwamba kazi ya wapelelezi hao haikuwa na ufanisi. Watu hao hawakufanikiwa kufichua kuenea kwa itikadi kali wala dhamira ya kufanya mauaji.
Gazeti la General Anzeiger linasema katika maoni yake kwamba sasa ni juu ya Mahakama Kuu kuingilia kati baada ya idara ya ulinzi wa katiba kushindwa kufanya kazi yake.Gazeti hilo linasema kuwa Mahakama Kuu ndiyo sasa inayopaswa kuamua kwa haraka ili kuepusha maafa makubwa zaidi. Naye mhariri wa Ostsee-Zeitung anasema panahitajika matayarisho mazuri ili kufanikiwa katika lengo la kuwapiga marufuku mafashisti mamboleo.
Mhariri huyo anaeleza kuwa Idara za Serikali sasa zinapaswa kuyatumia matukio ya hivi karibuni kama msingi wa kuzitayarisha hatua nyingine ili kukipiga marufuku chama cha mrengo mkali wa kulia- NDP. Ikiwa idara za serikali zitashindwa tena kukipiga marufuku chama hicho kwenye Mahakama Kuu, basi chama hicho kitapata nguvu mpya.! Lakini kwanza ni lazima kuwaondoa kabisa wapelelezi maalumu waliokuwa wanatumiwa na idara ya ulinzi wa katiba.
Mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten anasema kutumiwa kwa makachero hao maalumu hakukuleta manufaa katika harakati za kupambana na makundi yanayoenda kinyume na katiba. Gazeti hilo linaeleza kwamba muundo wa Idara ya ulinzi wa katiba unapaswa kufanyiwa marekebisho. Kazi zake, kwa kushirikiana na Polisi lazima ziimarishwe ili ziwe na ufanisi. Awali ya yote makachero maalumu waliokuwa wanatumiwa na idara ya ulinzi wa katiba watapaswa kuondolewa.
Kwa sababu kuwapo kwao hakukuleta usalama zaidi bali ni kinyume chake! Kwa hiyo gazeti hilo linasema watu wana haki ya kuuliza iwapo wapelelezi hao bado waendelee kupenyezwa katika makundi ya mafashisti mamboleo ili kuyapeleleza. Serikali inayoongozwa katika msingi wa katiba asilani haikihitaji chombo kisichokuwa na manufaa na hasa ikiwa chombo hicho kinazuia kazi zake.
Mwandishi/Mtullya abdu/ Deutsche Zeitungen/
Mhariri: Abdul-Rahman