Mapigano kusitishwa Pakistan baada ya watu 82 kuuliwa
25 Novemba 2024Maafisa wa Pakistan wametangaza siku saba za usitishaji mapigano baada ya mapambano makali ya risasi kati y amakabila katika wilaya ya Kurram, kaskazini magharibi mwa nchi, ambayo yamesababisha watu kiasi 82 kuuwawa na wengine 156 kujeruhiwa.
Msemaji wa serikali ya mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, Muhammad Ali Saif, amesema pande hizo mbili zimeafikiana kuhusu kusitisha mapigano kwa siku saba, ambapo wakati wa kipindi hicho watabadilishana wafungwa na kukabidhiana maiti za watu wao waliouwawa.
Afisa wa eneo hilo amesema juhudi zinafanywa kuwarejesha watu 20 ambao waliokuwa hawajulikani waliko pande zote mbili.
Machafuko yalizuka Alhamisi iliyopita wakati misafara miwili tofauti ya waislamu wa madhehebu ya Shia iliyokuwa ikisindikizwa na polisi iliposhambuliwa na waumini wapato 43 kuuwawa, na kuzusha makabiliano ya risasi ya siku mbili.