1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza karibuni kufikiwa

24 Januari 2024

Shirika la habari la Reuters linaripoti Israel na Hamas wanakaribia kufikia makubaliano juu ya kusimamisha mapigano kwa muda wa siku 30 kwenye Ukanda wa Gaza ambapo mateka wa Israeli na wafungwa wa Palestina wataachiwa

https://p.dw.com/p/4bdA2
Gaza, Khan Younis
Majeruhi wa mashambulizi ya Israel wakiwa katika Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis, Gaza.Picha: Belal Khaled/Anadolu/picture alliance

Qatar, Marekani na Misri zimekuwa zinafanya juhudi za kidiplomasia tangu mwezi Desemba ili kupunguza tofauti kati ya Israeli na Hamas kwa lengo la kuondosha uhasama, ili kuwezesha misaada zaidi ya kibinaadamu kupelekwa katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, pande hizo mbili bado zinatofautiana jinsi ya kuvimaliza kabisa vita vya Gaza, lakini Hamas imekataa kusonga mbele bila ya suala hilo kutatuliwa.

Msemaji  wa serikali ya Israel, Eylon Levy, amesema hakuna hatua ya kusimamisha mapigano itakayochukuliwa ambayo itawaachia Hamas waendelee kuwamo madarakani kwenye Ukanda wa Gaza na bila ya kuachiwa mateka wa Israel.