Makombora ya Urusi yawajeruhi watu 11 mjini Kharkiv
11 Januari 2024Urusi imefanya mashambulizi ya makombora yaliyopiga hoteli moja mjini Kharkiv, kaskazini mashariki mwa Ukraine na kujeruhi watu 11, wakiwemo waandishi wa habari.
Meya wa mji wa Kharkiv Igor Terekhov aliandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba mmoja wa majeruhi yuko katika hali mbaya na mwandishi wa habari wa Kituruki ni miongoni mwa walioumia.
Gavana wa kijeshi katika mji huo Oleh Syniehubov ameeleza kwamba jeshi la Urusi limeshambulia kwa kutumia makombora ya kukinga ndege aina ya S-300. Mashambulizi mengine yameripotiwa kwenye mikoa ya Donetsk na Dnipro-petrovsk.
Mapema jana, rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky alitoa wito wa kupatiwa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga, wakati alipokutana na Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda mjini Vilnius katika ziara ya siku mbili huko Baltiki.