1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamu wa rais wa Yemen awataka waasi kuheshimu serikali

16 Aprili 2015

Makamu mpya wa rais wa Yemen Khaled Bahah ametoa wito kwa wanajeshi waasi nchini humo kuwacha kuwaunga mkono waasi wa Kishia wanaopigana na serikali iliyoko uhamishoni.

https://p.dw.com/p/1F9Ya
Jemen Regierungschef Khaled Bahah ARCHIVBILD
Picha: Reuters/Khaled Abdullah

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, ambako anaishi uhamishoni pamoja na Rais Abedrabbo Mansour Hadi, makamu wa rais Khaled Bahah amewataka wanajeshi wote na vikosi vya usalama kukubali amri ya serikali halali na kuilinda nchi hiyo. Wanajeshi wanaomtii rais wa zamani Ali Adullah Saleh wameungana na waasi wa Kishia wa Houthi kupigana dhidi ya majeshi yanayomuunga mkono Rais Hadi.

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha mashambulizi ya kutokea angani mnamo Machi 26 dhidi ya wanajeshi waasi wanaoungwa mkono na Iran, katika vita vya udhibiti wa mji mkuu wa Yemen, Sanaa na kujikuta katika makabiliano makali na wanajeshi wanaomuunga mkono Hadi katika mji muhimu wa Kusini, wa Aden. Mazoezi ya kijeshi ya mataifa ya Kiarabu yanayopangwa nchini Saudi Arabia yameongeza uvumi kuwa muungano huo, unatafakari kuanzisha operesheni za ardhini.

Nchi wanachama wa muungano huo hazijafuta uwezekano wa kuwatuma wanajeshi wa ardhini nchini Yemen, lakini makamu wa rais Bahah amesema anatumai kuwa hilo halitahitajika.

Bahah ambaye pia anahudumu kama waziri mkuu, ametoa wito wa msaada wa dharura. Bahah pia ameipongeza Urusi kwa kutolizuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliweka marufuku ya silaha na vikwazo dhidi ya waasi wa Yemen.

Mazoezi ya kijeshi ya mataifa ya Kiarabu yanayopangwa nchini Saudi Arabia yameongeza uvumi kuwa muungano huo, unatafakari kuanzisha operesheni za ardhini. Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limesema takribani watu 736 wameuawa katika mgogoro huo kufikia Aprili 12 na zaidi ya 2,700 wamejeruhiwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu