Makamu wa rais wa Marekani kuzuru Afrika
13 Machi 2023Marekani inajaribu kuimarisha ushirika wake na Afrika, katikati ya ushindani mkali na nchi nyingine hususan China.
Taarifa kutoka kwa msemaji wake, Kirsten Allen, imeeleza kuwa ziara hiyo itaimarisha ushirikiano kati ya Marekani na mataifa kote Afrika na kukuza juhudi za kimaendeleo, kiusalama, kiuchumi na ustawi.
Miongoni mwa nchi anazotarajiwa kuzuru ni Ghana, Tanzania na Zambia.
Ziara hiyo itafuata ziara aliyofanya mke wa rais Joe Biden, Jill Biden na waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen. Aidha waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kuzuru Afrika wiki hii, huku rais Joe Biden akitarajiwa kuzuru mwishoni mwa mwaka.
Juhudi za ikulu ya White House kufikia bara la Afrika zilianza na mkutano wa kilele kati ya Marekani na viongozi wa Afrika mwezi wa Disemba.
China imewekeza pakubwa barani Afrika lakini Marekani inajipanga kama mshirika bora kuliko China.