1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamu wa Rais wa Kenya aapa kutojiuzulu

Thelma Mwadzaya25 Agosti 2021

Nchini Kenya, mzozo wa maneno kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto umechukua mkondo mpya baada ya Ruto kushikilia kuwa hatojiuzulu kwa vyovyote vile.

https://p.dw.com/p/3zSwm

Haya yanajiri saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutamka hadharani kuwa iwapo naibu wake hana raha basi na ajiondoe serikalini.

Naibu wa rais William Ruto amemjibu kiongozi wa taifa na kushikilia kuwa hatojiuzulu kwa vyovyote vile na kwamba hatotishwa kwani yuko kazini kutimiza maslahi ya wakenya.Aliyasema haya alipohudhuria maziko katika kaunti za Taita Taveta na Kwale saa chache zilizopita.

Wakati huohuo wabunge wanaomuunga mkono William Ruto wamemtaka rais Uhuru mwenyewe kujiuzulu kwa kumtenga naibu wake na sasa kumlaumu kwa tofauti zao.

Kwa upande wa pili, wanaomuunga mkono rais Uhuru Kenyatta wanamshinikiza naibu wa rais William Ruto ajiuzulu, wakidai ameshindwa kufanya kazi na kiongozi wa taifa.

Vuta nkuvute wakati wabunge wajadili vipengele vya BBI

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Uhusiano kati ya rais Kenyatta na makamu wake William Ruto umekuwa wa kusuasuaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Yote hayo yakiendelea, wabunge wanajiandaa kurejea vikaoni kuvipa ridhaa baadhi ya vipengele visivyohitaji kura ya maoni vilivyokuwamo kwenye mchakato wa maridhiano wa BBI uliobwagwa na mahakama ya rufaa wiki iliyopita.

Wabunge hao wameteua vipengee 52 vya mapendekezo ya BBI ili kuvipitisha.Dhamira ni kuvipa ridhaa kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 2022.

Vipengele hivyo ni pamoja na kuhakikisha kuwa 35% ya bajeti inatengewa serikali za kaunti, kuiongeza idadi ya maeneo bunge kwa kuteua 70 mapya pamoja na kuviruhusu vyama vya siasa kuteua wagombea wa urais na wenza kuwa mstari wa mbele kwenye orodha hiyo.

Kimsingi,mabadiliko ya katiba yanaweza kufanyika kupitia ridhaa ya bunge badala ya kura ya maoni inayohitaji ushiriki wa umma inapendekeza kamati ya utekelezaji wa katiba.

Kwa sasa,kulingana na katiba mchango wa umma unapewa uzito zaidi. Kadhalika azma yao ni kuiondoa haja ya mabunge yote 47 ya kaunti kujadili miswada muhimu na kupata ridhaa ya 24 kabla ya kupitishwa.Masuala hayo yamezua mitazamo tofauti kati ya wabunge.

Ifahamike kuwa hatima ya uchaguzi mkuu ujao haijakuwa bayana baada ya mahakama moja kuamuru kuwa tume ya uchaguzi na mipaka haijatimiza vigezo vya utendaji.