1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamu wa rais Iraq apinga hukumu ya kifo dhidi yake

Admin.WagnerD10 Septemba 2012

Makamu wa rais wa Iraq Tareq al-Hashemi amepinga hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi yake na mahakama nchini humo jana kwa makosa ya kuhusika na kupanga mauaji na kujigamba kwamba hukumu hiyo ni kama medali kifuani mwake.

https://p.dw.com/p/165yX
Makamu wa rais wa Iraq, Tareq al-Hashemi.
Makamu wa rais wa Iraq, Tareq al-HashemiPicha: picture-alliance/dpa

Makamu huyo wa rais ambaye ni moja wa waumini wa madhehebu ya sunni wenye vyeo vya juu kabisaa katika serikali ya Iraq amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara, Uturuki kuwa anaipinga hukumu hiyo kwa vile kesi iliyofunguliwa dhidi yake ilichochewa kisiasa, na kumshtumu waziri mkuu Nouri al-Maliki kwa ukandamizaji dhidi ya waumini wa madhehebu ya sunni.

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ambaye Hashemi anamshtumu kwa kumuandama kisiasa.
Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ambaye Hashemi anamshtumu kwa kumuandama kisiasa.Picha: AP

"Nakataa kabisaa, na kamwe sintotambua hukumu hiyo isiyo ya haki na yenye malengo ya kisiasa, ambayo ilitarajiwa tangu mwanzo wa kesi hii ya kuchekesha. Naichukulia hukumu hii kama medali kifuani mwangu, na gharama ya haki ambayo napaswa kulipwa kwa utumishi wangu uliyotukuka kwa nchi yangu Iraq na kwa wantu wangu, raia wa Iraq," alisema hashemi.

Hatari ya kuongezeka kwa vurugu za kidini
Wachambuzi wanasema hukumu hii inaweza kuchochea zaidi vurugu za kidini, baada ya siku mbaya ya mauaji ambapo watu wasiyopungua 88 waliuawa katika matukio mfululizo ya uripuaji wa mabomu. Hashemi aliikimbia Iraq baada ya mamlaka kutoa waranti wa kukamatwa kwake mwezi Desemba katika hatua ambayo ilitishia kuvunja makubaliano ya kugawana madaraka kati ya washia, wasunni na Wakurdi wakati ambapo majeshi ya Marekani yalikuwa yakiondoka nchini humo.

Hashemi alimshtumu waziri mkuu wa Iraq, Nouri al Maliki ambaye ni muumini wa madhehebu ya Shia, kwa kuendesha kampeni ya ukandamizaji dhidi ya waumini wa sunni na alikataa kuhudhuria katika mahakama ambayo alisema inaegemea upande. Yeye na mkwe wake ambaye pia ni katibu wake, walikutwa na hatia ya mauaji na mwanasheria wa kike na afisa usalama, Abdul Sattar al-Birqdar.

Mbunge kutoka chama cha Iraqiya kinachoungwa mkono na wasunni, Jabar al-Jaberi aliilezea hukumu dhidi ya Hashem ambaye ni kiongozi wa chama hicho,kuwa ya kisiasa zaidi. Wakili wa Hashemi alisema hawataka rufaa kwa sababu kesi imeendeshwa bila mteja wake kuwepo.

Uharibifu uliyofanywa kufuatia mirupuko mfululizo nchini iraq siku ya Jumapili.
Uharibifu uliyofanywa kufuatia mirupuko mfululizo nchini iraq siku ya Jumapili.Picha: Reuters

Serikali ya Nouri al-Malik katika mkwamo wa kisiasa
Tangu kuondoka kwa majeshi ya Marekani, serikali ya waziri mkuu Nouri al-maliki inayoogozwa na washia imekabiliwa na mkwamo wa kisiasa huku wanamgambo wakizidi kufanya mashambulizi, ambayo yanaweza kurudisha vurugu za kiitikadi zilizotishia kuipeleka nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2006 na 2007. Saa chache kabla ya hukumu hiyo kutolewa, mfululizo wa miripuko ulianza kuitikisa Iraq,kuanzia mji wa kaskazini wa Kirkuk hadi wa Nassiriya, kusini mwa Iraq ambako bomu lililotegwa kwenye gari lilishambulia jengo la ubalozi wa Ufaransa.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mabomumengine manne ya kwenye gari yalitika maeneo yanayokaliwa na washia wengi katika mji mkuu wa Baghdad, na kuua watu wasiyopungua 24. Mripuko mkali zaidi ulitokea karibu na mji wa Amara, kilomita 300 kusini mwa Baghdad ambako mabomu mawili yaliyotegwa kwenye gari yaliripuka nje ya eneo takatifu la washia na sokoni na kuua watu wasiyopungua 16.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afp,dpa
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman