1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majonzi nchini Kenya kufuatia mauaji ya al-Shabaab

Saumu Mwasimba19 Januari 2016

Miili ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) waliouwawa nchini Somalia imepokelewa kwa heshima zote za kijeshi nchini Kenya huku operesheni kubwa ya kuwakomboa wenzao walionusurika ikiendelea.

https://p.dw.com/p/1Hfnw
Rais Uhuru Kenyatta akihutubia taifa baada ya mkasa wa mauaji dhidi ya wanajeshi wa nchi hiyo kusini magharibi mwa Somalia.
Rais Uhuru Kenyatta akihutubia taifa baada ya mkasa wa mauaji dhidi ya wanajeshi wa nchi hiyo kusini magharibi mwa Somalia.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Raychelle Omamo, ndiye aliyeongoza ujumbe wa serikali katika kuzipokea maiti za wanajeshi hao zilipowasili kwenye uwanja wa ndege jijini Nairobi huku pia kukifanyika utaratibu maalum wa kutoa heshima za kijeshi.

Akizungumza kwa huzuni kubwa, Omamo aliwaomba Wakenya waendelee kuwa na subira wakati shughuli za kuwakomboa wanajeshi wengine zikiendelea. Alisema pia juhudi za kuipata miili zaidi ya wanajeshi waliouwawa zinaendelea ili nayo irejeshwe nyumbani kwa mazishi rasmi.

''Huu ni wakati wa majonzi kwa Jeshi la Kenya na kwa taifa letu kwa ujumla. Kwa mara nyingine, tungependa kutoa shukurani zetu kwa Wakenya wanaotuunga mkono kwa upendo wao katika kipindi hiki kigumu, kwa wanajeshi wetu na familia zao. Kama nilivyowaeleza awali, shughuli ya kuwatafuta na operesheni ya uokozi zinaendelea na tunatarajia kuwapokea wanajeshi wetu zaidi kadri siku zinavyokwenda.''

Hata hivyo, waziri huyo wa ulinzi hakutoa idadi kamili ya wanajeshi wa KDF waliouwawa, ingawa ameweka wazi kwamba wanategemea maiti zaidi. Kambi ya Jeshi la Umoja wa Afrika (AMISOM) kusini magharibi mwa Somalia ilishambuliwa na wapiganaji wa al-Shabaab mapema Ijumaa, likiwa ni tukio la hivi karibuni kabisa kwa AMISOM kushambuliwa ndani ya Somalia.

Wanamgambo wa al- Shabaab katika mji wa bandari wa Kismayu kabla ya kufurushwa na wanajeshi wa Kenya.
Wanamgambo wa al- Shabaab katika mji wa bandari wa Kismayu kabla ya kufurushwa na wanajeshi wa Kenya.Picha: picture-alliance/dpa

Al-Shabaab yadai kuuwa wanajeshi 100

Licha ya serikali ya Kenya kutosema idadi ya wanajeshi wake waliouwawa, kujeruhiwa au kutoweka, siku ya Jumapili kundi hilo la al-Shabaab lilitoa taarifa likisema zaidi ya wanajeshi 100 wa Kenya waliuwawa na wengine kushikiliwa mateka.

Katika taarifa yake, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kundi hilo halitopata muda wa kupumua, huku akiapa kwamba nchi yake italipiza kisasi ingawa haijafahamika hadi wakati huu ikiwa wanajeshi wa KDF walioko Somalia wameifikia kambi hiyo inayoshikiliwa na wanamgambo wa al-Shabaab.

Kadhalika, al-Shabab limetoa kanda mbili za sauti zilizorekodiwa likidai wanajeshi kadhaa wanashikiliwa mateka, na tovuti zao ndani ya Somalia zikitaja wanajeshi 12 kuwa ndio wanaoshikiliwa.

Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Sharmake, amelaani mashambulizi hayo akisema ni kitendo cha kinyama huku pia akituma salamu za rambirambi kwa familia za wanajeshi waliouwawa.

Umoja wa Ulaya, ambao ni mfadhili mkubwa wa kikosi cha AMISOM, umelaani pia mashambulizi hayo ukisema ni "jaribio jingine la kuuhujumu mchakato wa kisiasa kuelekea Somalia thabiti yenye usalama."

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman