Majimbo 16 ya Marekani yamfungulia mashtaka Trump
19 Februari 2019Mwanasheria Mkuu wa California Xavier Becerra ametoa taarifa rasmi hapo jana inayosema mashtaka hayo yanapinga hatua ya utawala wa Trump ambayo inakiuka sheria ya nchi hiyo.
Becerra ameongeza kwamba Rais Trump anautumia utawala wa sheria kwa kudharau kabisa, anajua hakuna mgogoro wa mpaka, anajua tamko la hali ya dharura ya taifa halikubaliki, na anakiri kwamba huenda akashindwa katika kesi hii ikifika mahakamani.
Wiki iliyopita akizungumzia ujenzi wa ukuta huo, Trump alisema kwamba chama cha Democratic kinampinga kwa sababu kinafikiri kufanya hivyo kutakisaidia kushinda uchaguzi ujao.
"Ninaweza kuujenga ukuta kwa kipindi cha muda mrefu. Sijakuwa na lazima ya kuchukua hatua hii ya haraka. Lakini ningependa kuujenga haraka. Na sina haja ya kufanya hivyo kwa ajili ya uchaguzi. Nishafanya vya kutosha kwa ajili ya uchaguzi wa 2020. Na sababu pekee tunalijadili suala hili ni uchaguzi. Wanatafuta ushindi wa uchaguzi, ambao inaonekana kama watashindwa. Na hii ni moja wapo ya njia wanayodhani inaweza kuwasaidia kushinda, kwa kuleta pingamizi na mengi yasiyokuwa na maana," alisema Trump.
Wanasheria wa majimbo yote 16 ni kutoka chama cha Democratic
Wanaoiunga mkono California ni wanasheria wakuu kutoka majimbo ya; Colorado, Connecticut, Delaware, Hawaii, Illinois, Maine, Maryland, Michigan, Minnesota, Nevada, New Jersey, New Mexico, New York, Oregon, na Virginia.
Majimbo yote yanayohusika na kesi hiyo yana wanasheria wakuu wanaotoka chama cha Democratic. Trump alitangaza hali ya dharura ya kitaifa ili kutimiza ahadi yake ya kujenga ukuta wa Mexico. Hatua hiyo itamruhusu rais kulikwepa bunge kutumia fedha kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon na bajeti nyingine.
Majimbo hayo yanasema utumiaji wa fedha za jeshi kujenga ukuta utaumiza uchumi na kuzinyima kambi za kijeshi kufanyiwa ukarabati unaohitajika. Majimbo hayo pia yanasema kuchukua fedha zilizotengwa kwa ajili ya juhudi za kupambana na madawa ya kulevya pia kutaleta matatizo. Majimbo ya California na New Mexico, yamesema ukuta huo anaotaka kuujenga Trump utawaathiri wanayama pori katika eneo hilo la mpakani.
Jimbo la California mara kwa mara limekuwa likimpinga Trump mahakamani. "Rais Trump ametengeneza mgogoro, na baadae kutangaza hali ya dharura ya kitaifa ya uwongo ili aweze kujiongezea madaraka na kukiuka katiba," amesema Gavana wa California Gavin Newsom katika taarifa yake. Gavana huyo ameongeza kwamba tangazao la Trump la hali ya dharura, ni kwa taifa zima.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap,afp
Mhariri: Josephat Charo