Majeshi ya Ufaransa yatabakia Afghanistan
20 Agosti 2008Sarkozy alietua mji mkuu wa Afghanistan Kabul leo asubuhi,alivizuru vikosi vya Ufaransa katika kambi yao nje ya mji huo mkuu na alitoa heshima za mwisho kwa wanajeshi 10 waliouawa.Vile vile aliwatembelea hospitalini wanajeshi 21 wa Kifaransa waliojeruhiwa katika mapigano na wanamgambo wa Taliban.Akasema kazi inayofanywa na wanajeshi ni muhimu,kwani uhuru wa eneo hilo upo hatarini.Akaongezea:
"Ninataka kuwaambieni kuwa ninatambua jukumu langu.Anaepitisha maamuzi ni miye.Mnapofikiwa na jambo,miye ndie dhamana.Kwa hivyo ni jambo la kawaida nikisema machungu yenu ni yangu."
Wanajeshi hao 10 waliuawa katika mapigano makubwa yaliyozuka baada ya kikosi cha Kifaransa kilichokuwa kikifanya doria,kuvamiwa na wanamgambo wa Taliban siku ya Jumatatu kiasi ya kilomita 50 kutoka Kabul.Mapigano hayo yamesababisha wasiwasi kuwa wanamgambo wa Taliban pole pole wanaukaribia mji mkuu Kabul.
Mwaka huu Rais Sarkozy alipeleka Afghanistan wanajeshi 700 ziada akiitikia mito ya Marekani kwa washirika wake wa NATO kutoa misaada zaidi kupambana na waasi wa Taliban.Hivyo,Ufaransa ikawa na kama wanajeshi 3,000 nchini Afghanistan.Uamuzi huo ulipingwa na wengi nchini Ufaransa,kwa sababu ya kuhofia kuwa wanajitumbukiza katika vita visivyokuwa na mwisho.Kufuatia vifo hivi vipya,kiongozi wa chama cha upinzani cha Kisoshalisti nchini Ufaransa,Francois Hollande amesema,umma lazima uelezwe kile kinachofanywa na wanajeshi wa Ufaransa huko Afghanistan na vile vile muda watakaobakia huko.
Kama wanajeshi 70,000 wa kimataifa wanashirikiana na majeshi ya Kiafghanistan kupigana dhidi ya wanamgambo wa Taliban walioondoshwa madarakani katika uvamizi ulioongozwa na Marekani,kufuatia mashambulizi ya Septemba mwaka 2001.
Mashambulizi ya Jumatatu na Jumanne ni mabaya kabisa kupata kufanywa dhidi ya majeshi ya Ufaransa tangu vikosi hivyo kupelekwa Afghanistan. Sasa idadi ya wanajeshi wa Kifaransa waliouawa tangu Ufaransa kwa mara ya kwanza kupeleka majeshi yake Afghanistan mwaka 2002 imefikia 24.