Majeshi ya Iraq yaelekea kuukomboa mji wa Mosul
25 Juni 2017Vikosi vilivyopewa mafunzo na Marekani katika vita vya mjini vinaendelea na mapambano yake katika mitaa miwili muhimu ambayo inakutana katikati ya mji huo mkongwe, kwa lengo la kuwatenga wanamgambo wa jihadi katika maeneo madogo madogo manne.
Mapambano hayo yaliyodumu kwa wiki moja sasa katika mji huo mkongwe yanafikia sasa mapigano makali mno katika kampeni ya miezi minane hivi sasa inayoungwa mkono na Marekani kuukomboa mji huo wa kaskazini, ambao uliangukia mikononi mwa wanamgambo Juni , 2014.
Mwandishi habari wa shirika la habari la Reuters alimuona msichana mdogo akiwa na majeraha usoni akitembea akiwa amechoka akipita mstari wa mbele wa mapambano kutoka katika wilaya yenye watu wengi akiwa na kundi la majirani. Familia yake yote imeuwawa wakati nyumba yao ilipoanguka, wanasema.
Umoja wa mataifa umeeleza hali ya hatari jana Jumamosi kwa idadi kubwa ya vifo vya raia katika mapigano, ukisema zaidi ya watu 12 waliuwawa na mamia wamejeruhiwa siku ya Ijumaa.
Mapigano makali
"Mapigano ni makali mno katika mji mkongwe na raia wako katika hali mbaya, na hatari ambayo haina mfano. Kuna ripoti kwamba maelfu, huenda hata mamia kwa maelfu , ya watu wanashikiliwa kama ngao ya binadamu na wanamgambo wa Dola la Kiislamu," Lise Grande , mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa mataifa nchini Iraq, amesema katika taarifa. "Mamia ya raia , ikiwa ni pamoja na watoto, wanapigwa risasi."
Maafisa nchini Iraq wanamatumaini ya kutangaza ushindi katika mji huo wa kaskazini mwa Iraq katika wakati wa sikukuu ya Eid , ambayo ni kuadhimisha mwisho wa mfungo mtukufu wa Ramadhan, katika siku chache zijazo.
Helikopta zenye silaha zilikuwa zinasaidia mapambano ya vikosi vya ardhini , zikishambulia maeneo waliko wanamgambo katika mji mkongwe, mwandishi wa shirika la ndege la Reuters ameripoti kutoka katika eneo karibu na mstari wa mbele wa maambano.
Kusongambele kwa majeshi ya serikali kunatengeneza njia za kupita raia wakikimbia kutoka katika maeneo yanayoshikiliwa na kundi la Dola la Kiislamu.
Raia wanakimbia mapigano
Kumekuwa na mmiminiko taratibu wa familia zinazokimbia jana , baadhi wakiwa wamejeruhiwa pamoja na watoto ambao wamedhoofu kwa njaa. "Mtoto wangu amekuwa akila mkate na maji kwa siku nane zikizopita," mama mmoja alisema.
Kiasi raia 100 waliwasili salama katika eneo linaloshikiliwa na serikali magharibi mwa mji mkongwe katika kipindi kimoja cha dakika 20, wakiwa wamechoka, wakiwa na hofu na njaa. Wanajeshi waliwapa chakula na maji.
Zaidi ya raia 100,000 , miongoni mwao nusu wanaaminika kuwa ni watoto, wanaendelea kunaswa katika majengo ambayo ni magofu katika mji huo mkongwe, wakiwa hawana chakula, maji ama matibabu.
Majeshi yanayopigana vita vya mjini yanaongoza kampeni kusafisha eneo hilo kuwaondoa wapiganaji kutoka katika mitaa kadhaa ya mji huo mkongwe, wakitembea kwa miguu nyumba kwa nyumba katika maeneo yaliyojaa vifusi na kuwa taabu kwa magari ya kivita kupita.
Mwandishi habari raia wa Ufaransa Veronique Robert alifariki mjini Paris baada ya kujeruhiwa katika mripuko mjini Mosul maema wiki hii, mwajiri wake televisheni ya Ufaransa amesema siku ya Jumamosi. Bomu liliripuka na kumuua mwandishi habari wa Iraq Bakhtiyar Haddad na mwandishi habari wa Ufaransa Stephane Villenueve wakati mwandishi mwingine wa kujitegemea alipata majeraha madogo.
Mashirika ya kutoa misaada na maafisa wa Iraq wanasema kundi la Dola la Kiislamu linawazuwia raia kutoka ili kuweza kuwatumia kama ngao ya binadamu. Mamia ya raia wanaokimbia kutoka mji mkongwe wamepigwa risasi na kuuwawa katika wiki tatu zilizopita.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusra Buwayhid