Majeshi ya Gaddafi 'yajiondoa' Misrata
26 Aprili 2011Serikali ya Libya imesema kuwa kuondoka kwa majeshi yake kutoka mji wa Misrata, hakutokani na kushindwa na waasi, bali kuwaachia wakaazi wa mji huo kumaliza matatizo yao kisiasa na sio kijeshi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Khaled Kaim, hivi sasa jeshi limesitisha operesheni yake, lakini linaendelea kubakia kuwaruhusu viongozi wa kikabila kutatua mgogoro uliopo baina ya pande mbili kwa njia za amani.
Kwa wiki ya saba sasa, mji huo umezingirwa na majeshi ya Gaddafi, huku mashambulizi baina yake na waasi yakisababisha vifo na majeruhi kadhaa, wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida, hasa wanawake, wazee na watoto.
Pamoja na kauli hiyo ya serikali, bado mizinga na bunduki zimekuwa zikisikika kutokea upande wa majeshi yake. Lakini msemaji wa serikali ya Gaddafi, Musa Ibrahim, anasema majeshi hayo hayashambulii tena, isipokuwa hujilinda pale yanaposhambuliwa.
"Wakati wanajeshi wetu walipokuwa wakijiondoa Misrata, waasi waliwashambulia, na wanajeshi wetu wakarudisha mashambulizi. Lakini limeendelea kujiondoa mjini. Bila ya shaka, tukishambuliwa, tutajibu, maana sisi sio woga." Amesema Ibrahim.
Urusi yapinga hatua zaidi za kijeshi
Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema nchi yake haitakubaliana na azimio lolote la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, litakalotaka uingiliaji wa majeshi ya kigeni nchini Libya.
Kauli hii inakuja, baada ya Uingereza, Ufaransa na Italia kutaka hatua kali zaidi zichukuliwe, kwa kile wanachokiita "kuwalinda raia" dhidi ya majeshi ya Gaddafi.
Licha ya operesheni ya kijeshi inayoongozwa na NATO kukaribia mwezi mzima sasa, bado raia wanaendelea kushambuliwa. Urusi ilijizuia kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio lililoruhusu operesheni hii, lakini sasa inasema itazuia maazimio mengine yanayoihusu Libya, isipokuwa tu yale yatakayotaka usitishaji wa mara moja wa umwagaji damu na matumizi ya nguvu za kijeshi.
Italia na Ufaransa zafikia makubaliano
Kwa upande mwengine, Italia imekubali kutoa ndege zake kushiriki kwenye operesheni ya NATO nchini Libya. Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, baada ya mazungumzo yake na Rais Nicolas Sarkuzy wa Ufaransa leo hii mjini Rome.
Viongozi hao pia wametoa wito wa pamoja wa kuitaka jumuiya ya kimataifa iache kununua bidhaa zote za mafuta kutoka serikali ya Gaddafi.
Kuhusu suala tete la wakimbizi wa Afrika ya Kaskazini wanaoingia kwa wingi barani Ulaya, kupitia kisiwa kinachomilikiwa na Italia cha Lampedusa, Berlusconi na Sarkozy wameutaka Umoja wa Ulaya kuufanyia marekebisho mkataba wa visa, ili uyaruhusu mataifa wanachama kuweka udhibiti kwenye mipaka yao.
Katika hali ya sasa, mkataba huo maarufu kama Schengen, unawaruhusu watu wote wanaoishi au kuingia kwenye moja ya nchi 25 zilizousaini, kusafiri na kuingia kwenye nchi yoyote waitakayo. Italia ilitumia ruhusa hiyo kuwapa vibali mamia ya wakimbizi, hatua ambayo imelalamikiwa na wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya, ikiwemo Ufaransa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji