Majeshi ya Ethiopia na Somalia kufanya msako mkubwa mjini Mogadishu
12 Novemba 2007Uamzi huo wa majeshi ya Ethiopia na yale ya mpito ya serikali ya Somalia umekuja baada ya mauaji ya watu zaidi ya 80 katika kipindi cha juma moja lililopita, yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo iliyoko kwenye pembe ya Afrika.
Msako huo unahusisha eneo la soko la Bakara ambapo kunasemekana kupatikana silaha za aina mbalimbali zinazowezesha mauaji ya raia kupitia mikono ya vikundi vya wapiganaji dhidi ya majeshi ya kigeni na yale ya serikali.
Hata hivyo shabaha kubwa ya waasi imekuwa ikiwalenga raia wa kawaida hasa wanawake na watoto, na hivyo kuuwa watu wasiokuwa na hatia.
Meya wa mji wa Mogadishu Bwana Mohamed Omar Habeb amenukuriwa akisema kwamba mtu yeyote atakayeshindwa kuwepo kwenye eneo lake la biashara atahesabiwa kuwa miongoni mwa watu wanaojihusisha na biashara ya kuuza silaha.
Eneo la soko la Bakara linasemekana kuwa maficho ya wapiganaji wenye itikadi kali na kwamba limegeuzwa kuwa soko kuu la biashara ya silaha zinazotumika kufanikisha mauaji ya kiraia nchini Somalia.
Hata hivyo mpango huo wa majeshi ya Somalia na Ethiopia umepingwa na baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo kwa madai kwamba wanahofia biashara zao kuibwa au kuporwa wakati wa msako huo.
Mkuu wa chama cha wafanyabiashara katika soko la Bakara mjini Mogadishu Bwana Mohamed Siad amesema wao hawapingi kufanyika msako huo, ila wameomba kutoharibiwa au kuibiwa biashara zao nyingine wanazofanya kwa njia halali na kuwaingizia kipato.
Ameongeza kwa kusema kwamba japo haamini kwamba soko hilo lina wafanyabiashara wanaouza silaha, majeshi hayo yanaweza kufanya lolote lililokusudiwa bila kuwabugudhi wafanyabiashara wala kuwasababishia hasara yoyote.
Msako huo wa silaha umekuja wakati ambapo mapigano makali yametokea karibu na makazi ya Rais kwenye eneo la kusini mwa Mogadishu linalosemekana kuwa hatari zaidi kwa usalama wa raia, lakini hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa.
Kufuatia tukio hilo lililotokea saa chache zilizopita, Mamala za serikali ya Somalia zimewatia mikononi baadhi ya wana itikadi kali wanaosemekana kuhusika katika mashambulizi hayo, akiwemo msemaji wa wapiganaji Bwana Ahmed Diriye, watoto wake wawili na kiongozi mwingine wa makamo.
Hata hivyo Bwana Mohamed Hassan Haad ambaye ni mkuu wa ukoo wa Hawiye amesema watu hao wamekamatwa kimakosa kwa vile hawana makosa yoyote na ametaka waachiwe mara moja.
Takwimu zinaonesha kwamba mauji ya kutisha yamefanyika mwishoni mwa juma lililopita ambapo zaidi ya watu 80 wengi wakiwa raia wa kawaida walipoteza maisha, tangu majeshi ya Ethiopia yalipokwenda nchini Somalia miezi saba iliyopita.
Wakati mauaji hayo yakitisha nchini Somalia, pia idadi ya wakimbizi imepanda hadi kufikia elfu 90 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.