Majeshi ya AMISOM yaingia rasmi Kismayu
2 Oktoba 2012Msemaji wa Jeshi la Kenya katika operesheni hiyo Emanuel Chirchir ameiambia DW kwa njia ya simu kwamba majeshi ya Umoja wa Afrika na yale ya Somalia yameuzunguka mji wa Kismayuu na pia kuidhibiti bandari ya mji huo wa kusini.
Chirchir amesema wakati majeshi hayo yakiingia mji wa Kismayuu, watu walitoka nje ya nyumba zao na kushangilia kwa kupiga makofi kuonesha kuunga mkono hatua hiyo.
Akijibu suala iwapo majeshi hayo yatafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwakamata al-Shabaab, Chirchir alisema wakaazi wa Kismayuu wengi wanajishughulisha na biashara na kwamba hawaoni haja ya kuingia kwenye nyumba kufanya msako kama huo.
Kismayuu ilianguka bila upinzani mkali
Alisema wanajeshi wa majeshi ya Afrika na Somalia waliokuwa Kaskazini Magharibi mwa mji waliingia bila ya purukushani zozote ndani ya mji na wanaelekea uwanja wa ndege ambapo kwa sasa hakuna matukio ya mashambulizi kwenye mji wa Kismayu na kwamba mji umetulia kabisa.
Akieleza kama anafahamu wapi Al shabab wamekimbilia kwa sasa Chirchir alisema wanadhani wanamgambo hao wapo katika eneo la Barawe na kwamba vikosi vya Jeshi la Umoja wa Afrika na Somalia vitafika huko.
Alisema zipo taarifa kuwa wanamgambo hao wanataka kujisalilimisha, nao wametoa wito kwa wanamgambo hao kufanya hivyo.
Siku ya Jumatatu kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni al-Shabaab walirusha kombora kwenye kituo cha polisi cha Garissa kilicho karibu na mpaka wa Somalia,ambapo siku moja kabla polisi wawili waliuawa baada ya kushambuliwa kwa risasi katika mji huo.
Mkuu wa Wilaya ya Garissa Mohammed Maalim alisema kombora la kurushwa kwa mkono liliripuka lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa na mashambulizi ya silaha kati ya kundi la Alshabab na yale ya Afrika na Somalia yaliweza kudumu kwa muda wa dakika kumi wiki iliyopita.
Kuondoshwa kwa wanamgambo wa kundi la al-Shabaab mjini Kismayu inaweza kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha usalama katika eneo hilo ambalo limekuwa mara kadhaa katika vita isiyokwisha.
Marekani yawapongeza AMISOM
Kwa upande wake Marekani imeyapongeza majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Kenya kwa kulikimbiza kundi la al-Shabaab nchini Somalia katika bandari ya Kismayu na kuwataka viongozi wa Somalia kudumisha usalama katika bandari hiyo.
Mwanadiplomasia wa Marekani Barani Afrika Johnnie Carson aliwaelewa waandishi wa habari akiashiria katiba mpya ,bunge jipya na rais mpya wa Somalia kwamba Somalia ipo katika historia mpya baada ya miaka mingi ya ugoigoi.
Umoja wa Afrika wenye majeshi 17,000 nchini Somalia waliingia mji wa Kismayu siku ya Jumatatu na kuanza kuwafurusha nje ya mji huo wanakikundi cha al- Shabaab.
Marekani pia inaweka kipaumbele kwa kuisaidia serikali mpya ya Somalia katika vikosi vya ulinzi pia kuimarisha miundombinu wa taifa hilo la pembe ya Afrika.
Mwandishi: Khatib Mjaja/AFP/DW Kiswahili
Mhariri: Mohammed Khelef