Majeshi ya Afghanistan yaudhibiti mji mkuu
16 Aprili 2012Vikosi vya serikali ya Afghanistan ndivyo vilivyoongoza operesheni hiyo ya kuurudisha mji huo mkuu mikononi mwake, lakini msemaji wa jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO, amesema kwamba walitoa msaada kwa vikosi hivyo baada ya kuombwa kufanya hivyo. Watu 47 waliuwawa nchini Afghanistan katika mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa kundi lenye msimamo mkali wa Kiislamu, Taliban. Mashambulizi hayo yalifanyika katika mji mkuu Kabul na miji mingine mitatu kwa muda wa masaa 18.
Katika mkutano na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya ndani wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi alieleza kwamba mbali na kusababisha vifo vya watu 47, shambulizi la wataliban liliwajeruhi pia watu 65, 40 kati yao wakiwa maafisa wa usalama na 25 raia wa kawaida. Mohammadi alisema kwamba waasi 16 ndio waliofanya mauaji mjini Kabul. "Walipokuwa wakiingia mjini walikuwa wamevaa hijabu . Waliweka maua katika gari lao kuashiria kwamba wanakwenda kwenye sherehe," alieleza waziri huyo.
NATO yaisifu Afghanistan
Milio ya risasi ilianza kusikika Jumapili mchana katika miji ya Kabul, Jalalabad, Gardez na Logar. Kulitokea pia miripuko lakini baadaye wanajeshi wa Afghanistan walianza kujibu mashambulizi ambapo baadhi ya wapiganaji wa Taliban waliuwawa.
Kamanda wa jeshi la ISAF la kundi la kujihami la NATO, Jenerali John Allen, amewapongeza maafisa wa usalama wa Afghanistan kwa jinsi walivyopambana na waasi. "Walikuwa wamejipanga vizuri na kuongozwa vizuri na walitumia juhudi yao kulinda maisha ya raia wenzao," alisema Allen.
Naye mkuu wa polisi wa mji wa Kabul, Jenerali Ayoub Salangi, ameeleza kwamba watu 35 walitekwa na waasi karibu na jengo la Bunge la Afghanistan lakini hata hivyo watu hao baadaye waliweza kuokolewa. Kwa mujibu wa mkuu wa polisi, ni mwanamke mmoja tu aliyejeruhiwa.
Ubalozi wa Ujerumani washambuliwa
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amelaani mapigano yaliyotokea Afghanistan na kuahidi kwamba nchi yake itaendelea kuyaunga mkono maendeleo yanayofanyika Afghanistan. "Tutaendelea kupambana na uasi wa magaidi," alisema Westerwelle. Tutaendelea kusaidia kujenga Afghanistan yenye amani na yenye mazingira mazuri ya kuishi. Licha ya kuwekewa vikwazo,tutaendeleza sera yetu ya kulikabidhi jukumu la usalama wa nchi kwa raia ."
Ubalozi wa Ujerumani ni miongoni mwa majengo yaliyoshambuliwa katika mapigano yaliyoanza jana Jumapili. Hata hivyo Westerwelle ameeleza kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa katika ubalozi huo. Wafanyakazi wote walipelekwa mahali penye usalama.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef