1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majenerali Sudan wasitisha mapigano kwa siku saba

Josephat Charo
3 Mei 2023

Mzozo uliolipuka Aprili 15 huko Sudan umesababisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimisha wengine zaidi ya 100,000 kuhamia nchi nyingine. Mamia kwa maelfu wengine ni wakimbizi wa ndani.

https://p.dw.com/p/4QotW
Clashes continue in Sudan
Picha: picture alliance / AA

Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al Burhan na mkuu wa kikosi maalumu cha jeshi kinachopambana na jeshi la taifa, RSF, Mohammed Hamdan Daglo, wamekubaliana juu ya mkataba wa usitishwaji mapigano kwa siku saba kuanzia Alhamisi Mei 4 hadi Alhamisi wiki ijayo Mei 11. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini.

Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuanza mazungumzo ya upatanishi kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana, kama muwakilishi wa shirika la maendeleo la nchi za ukanda wa Afrika mashariki na pembe ya Afrika, IGAD. Kiir anatafuta kuyafikisha mwisho mapigano kati ya vikosi vya mkuu wa majeshi al Burhan na vile vya naibu wake Mohammed Hamdan Daglo anayekiongoza kikosi cha wanamgambo wa RSF.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini imesema Al-Burhan na Daglo wamekubaliana kuwataja wawakilishi kwa ajili ya mazungumzo yatakayofanyika katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Wizara hiyo imesema hakuna terehe iliyopangwa ya lini mazungumzo hayo yatakapoanza, lakini hali ya kibinadamu inayozidi kuendelea kuwa mbaya inaifanya kuwa vigumu kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano kwa saa 72 yameafikiwa tangu machafuko yalipozuka mnamo Aprili 15, lakini yamevunjwa mara kwa mara.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na mwenzake wa Misri Sameh Shoukry wamejadili kwa njia ya simu juu ya kuurefusha na kuutanua usitishwaji mapigano Sudan.

Krieg in Sudan | Kämpfe in Khartoum
Moshi mweusi ukitanda anga la mji wa Bahri unaojulikana pia kama Khartoum KaskaziniPicha: via REUTERS

Wakati hayo yakiarifiwa msemaji wa ikulu ya Marekani Karine Jean-Pierre amesema mashirika ya misaada sharti yaruhusiwe kuwafikia na kuwasaidia watu Sudan, huku mapigano zaidi yakiendelea kushuhudiwa nchini humo.

Kando na hayo naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Vedant Patel amesema ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah nchini Saudi Arabia umewakaribisha na kutoa huduma za kibalozi kwa raia zaidi ya 350 wa Marekani na wakaazi halali wa Marekani walioikimbia Sudan.

Machafuko yaendelea

Hapo jana watu walioshuhudia waliripoti juu ya mashambulizi zaidi ya kutokea angani katika miji ya Omdurman na Bahri, yote ikiwa upande wa pili wa ukingo wa mto Nile kutoka mji mkuu Khartoum. Jeshi la Sudan lilisema katika taarifa likinukuu ripoti ya balozi kwamba ubalozi wa India mjini Khartoum ulishambuliwa na kuporwa.

Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imesema mapema leo kwamba jengo la ofisi zake za ubalozi limevamiwa na kuporwa na kundi lililojihami na silaha. Hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa wala kuuliwa katika tukio hilo.

Madege ya kivita ya jeshi la Sudan yameendelea kuwashambulia wapiganaji wa kikosi cha RSF wanaoendesha mapambano katika maeneo ya makazi katika mji mkuu Khartoum. Machafuko pia yameenea hadi jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan ambako kikosi cha RSF kiliibuka kutoka kwa waasi wa kikabila waliopigana bega kwa bega na vikosi vya serikali kuwachakaza waasi katika vita vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe miaka 20 iliyopita.

(afp, reuters, dpa)