Majenerali wakamatwa Rwanda kwa kukiuka kanuni za corona
28 Aprili 2021Rwanda inaendelea na kamatakamata ya wanaokiuka masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, na safari hii wametiwa nguvuni Jenerali Fred Ibingira, Mkuu wa Jeshi la Akiba na Luteni Jenerali Charles Muhire ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Anga.
Soma pia Rwanda yapokea shehena yake ya chanjo ya corona
Ripoti za wananchi wa kawaida na viongozi wa serikali za mitaa kukamatwa kwa ukiukwaji wa masharti ya kuzuia kusambaa kwa Covid-19 zimekuwa zikisikika kila kukicha tangu kugundulika kisa cha kwanza cha maambukizi, lakini leo ndiyo mara ya kwanza wamekamatwa majenerali wa jeshi, kitendo kilichowashtua wengi kutokana na vyeo vyao vikubwa. Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda, Luteni Kanali Ronald Rwivanga ameithibitishia DW kuhusu kukamatwa kwa vigogo hao.
"Mmoja alihudhuria harusi huko Butare, namzungumzia Jenerali Ibingira, ilikuwa ni harusi ya watu zaidi ya sabini, haikubaliki, na kuhusu Jenerali Muhire, yeye alikwenda hoteli moja huko Rebero na kuchangia kinywaji na watu 33, hiyo pia haikubaliki. Wametiwa ndani na hatua stahiki zitachukuliwa kujua kama watakaa ndani kwa muda gani,” amesema Rwivanga.
Rwanda yaanza kutoa chanjo ya COVID-19
Makamanda wa polisi pia wakamatwa kwa kutowajibika
Lakini si majenerali hao wawili pekee ndio wamekamatwa bali wamekamatwa pia makamanda wakuu wa Jeshi la Polisi ambao, kwa mujibu wa Msemaji wa Polisi John Bosco Kabera, walikuwa na taarifa kuhusu vitendo vya majenerali hao lakini hawakuchukua hatua zozote wala kuripoti matukio hayo. Waliokamatwa ni Francis Muheto, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kusini, na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Huye Gaton Karagire.
Rwanda imesifika kimataifa kwa juhudi zake za kupambana na virusi vya corona ikiwa ndiyo nchi ya kwanza ya Afrika kutangaza marufuku ya kutotoka nje mwaka jana, tangu wakati huo wamekamatwa watu wengi na kutozwa faini lakini bado baadhi katika mitandao ya kijamii wameendelea kusema wanaogopa adhabu kuliko corona huku wengine wakisema hawaamini kwamba corona ipo. Msemaji wa Polisi John Bosco Kabera katika mahojiano na DW amesema watu hao wanajulikana lakini wanatakiwa wajielimishe.
"Watu hao tumekuwa tukisisitiza kwamba waogope corona waache kuogopa polisi maana corona ni tishio kwa dunia nzima siyo Rwanda tu, corona huua na kuyumbisha afya za watu, kwa hiyo watu wasiogope polisi badala yake watoe taarifa polisi kila waonapo vitendo vya watu wasiotii masharti ya kuzuia corona,” amesema Kabera.
Baraza la Mawaziri limekuwa likisasisha masharti ya kuzuia virusi vya corona kila baada ya wiki mbili, na masharti yaliyopo kwa sasa yanaruhusu harusi ila wasizidi watu ishirini huku baa zikiendelea kupigwa marufuku tangu Machi mwaka jana.