Majaji wa ICC wamuachia huru Gbagbo
15 Januari 2019Majaji hao, wakimvua dhamana ya jukumu la uhalifu uliotokea kufuatia mzozo wa uchaguzi mwaka 2010, wakisema upande wa mashitaka ulishindwa kutoa ushahidi wa kesi hiyo.
Jaji Cuno Tarfusser aliamuru kuachiwa huru mara moja kwa kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 73 Gbagbo pamoja na Ble Goude mwenye umri wa miaka 47 kufuatia hukumu hiyo ambayo imekuja kabla ya mawakili wao kutoa utetezi. Tarfusser amesitisha amri hiyo kabla ya kikao cha ufuatiliaji hapo kesho Jumatano.
Waendesha mashitaka wanaweza kukata rufaa. Katika taarifa ya maandishi , wameieleza hukumu hiyo kuwa "inakatisha tamaa na isiyotarajiwa" na kusema watafanya tathmini uamuzi huo ulioko katika maandishi wakati utakapochapishwa "na kutathimini hatua muafaka za kuchukua."
Gbagbo alikuwa rais wa kwanza wa zamani kufikishwa katika mahakama hiyo ya dunia na kesi yake ilionekana kama alama muhimu katika juhudi za kuwafikisha katika mikono ya sheria viongozi wa ngazi za juu wanaoshutumiwa kufanya mauaji.
Waendesha mashitaka washindwa kuthibitisha
Zaidi ya watu 3,000 waliuwawa baada ya Gbagbo kukataa kukubali kushindwa na hasimu wake na rais wa sasa wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara.
Tarfusser amesema wengi miongoni mwa majaji watatu katika jopo la majaji katika kesi hiyo wameamua kwamba "waendesha mashitaka wameshindwa kuthibitisha mzigo wa jukumu dhidi ya watu hao wawili.
"Mahakama baada ya kufanya tathmini ya kina kuhusu ushahidi na kutafakari kuhusu maelezo yote yaliyowasilishwa kwa mdomo na kwa maandishi kutoka pande zote na walioshiriki, imegundua kwa wingi wa majaji kwamba hakuna haja kwa upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi zaidi kwa kuwa waendesha mashitaka wameshindwa kutoa maelezo ya kutosheleza kuhusu ushahidi wa uhusiano wa mambo mbali mbali yahusuyo uhalifu kama ulivyowekwa katika mashitaka."
Jaji Tarfusser amesema ni muhimu kuweza kumbukumbu kwamba Cote d'Ivore ilivurugwa na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2010 na mapema 2011, lakini alisema waendesha mashitaka hawakuweza kuwasilisha ushahidi kwamba Gbagbo na Ble Goude walitayarisha mpango kwa waungaji wao mkono kufanya ghasia ili kumuweka Gbagbo madarakani.
Gbagbo na Ble hawakuzungumza mahakamani na wakili wa Gbagbo Emmanuel Altit aliuita kuwa ni ushindi kwa sheria.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Iddi Ssessanga