Majaji Kenya wajadili uhuru na uadilifu
28 Julai 2021Kwenye kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya kielektroniki kilichoandaliwa na kamati ya kumbukumbu ya Jaji K.T Desai, majaji hao walibadilishana mawazo chini ya uongozi wa Jaji mstaafu wa kwanza wa kike wa mahakama kuu ya Bombay na ile ya juu ya India, Sujata Manohar.
Suala la anayepaswa kuwa na kauli ya mwisho wakati wa kuwateua majaji wa mahakama ya juu lilitawala na mitazamo tofauti ilijitokeza jukwaani.
Kikao hiki kinafanyika wakati ambapo vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti mgongano kuhusu uhuru wa idara ya mahakama na wajibu wa bunge la taifa.
Katika kipindi cha wiki chache zilizopita Jaji Mkuu nchini Kenya Martha Koome aliwasilisha waraka maalum kwa maspika wa bunge la taifa na baraza la senate kutambua wajibu wao wa uelekezi katika taasisi za umma.
Azma yake ni kuwa na kikao cha pamoja cha kujadili suala la muingiliano pale kamati mbalimbali za bunge na baraza la senate zinapowasilisha notisi kwa idara ya mahakama.
Katika kisa kimoja alichotolea mfano Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome, Mratibu mkuu wa Idara ya mahakama alitazamiwa kufika mbele ya kamati tatu za bunge la taifa na baraza la senate katika siku hiyo hiyo moja.
Soma pia: Kenya: Ukiishi na mpenzi bila ndoa marufuku kurithi mali
Umuhimu wa uwiano kati ya mahakama na bunge
Jaji Mkuu Martha Koome alisitiza umuhimu wa kuwa na uwiano na uhusiano mzuri kati ya bunge la taifa na idara ya mahakama.
Suala la kesi kusuasua nalo pia limeifanya idara ya mahakama kunyoshewa kidole cha lawama. Hata hivyo Jaji Mkuu Martha Koome amesema kuna mabadiliko kwenye namna majaji wanavyoandaa hukumu zao na wanahitaji mafunzo ya ziada.
Hata hivyo Spika wa Bunge la Taifa nchini Kenya Justin Muturi alishikilia kuwa wabunge wana wajibu wa kuzisimamia mahakama na kwamba kamati za bunge nazo zina mamlaka ya kutoa notisi na kuwaita wanaohitaji kujibu maswali mbele yao.
Itakumbukwa kuwa siku chache zilizopita majaji Saidi Chitembwe na Aggrey Muchelule walivamiwa na kukamatwa na maafisa wa usalama afisini mwao, lakini ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu Noordin Haji imekanusha kuhusika katika kadhia hiyo.
Jaji Saidi Chitembwe alijitosa kwenye kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya Jaji Mkuu mapema mwaka huu bila mafanikio. Kikao cha Jumatano kimesitiza umuhimu wa kudumisha uadilifu na uhuru wa mahakama chini ya muongozo wa katiba.
Mkutano huo pia uliwaleta pamoja Sharad Rao ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya uhakiki wa majaji na mahakimu nchini Kenya, Jan van Zyl Smit wa kituo cha sheria cha Bingham cha London na Arvind Datar,wakili wa ngazi ya juu huko India