Majadiliano ya kugawana madaraka Zimbabwe
12 Agosti 2008Majadiliano hayo kati ya chama tawala cha ZANU-PF na MDC cha upinzani yanafanywa chini ya upatanishi wa Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare.Siku ya Jumatatu,Rais Mugabe kufuatia majadiliano ya siku mbili pamoja na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai na vile vile kiongozi wa tawi lililojitenga na MDC,Arthur Mutambara,aliwaambia waandishi wa habari maendeleo fulani yamepatikana.Lakini afisa mmoja wa ZANU-PF amenukuliwa akisema,mazungumzo hayo yapo hatarini.
Kwa upande mwingine,waachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema,Arthur Mutambara wa tawi la MDC huenda akawa na umuhimu mkubwa katika majadiliano ya kugawana madaraka.Kwani wabunge wa tawi hilo wanaweza kuimarisha bungeni chama cha Mugabe ZANU-PF au chama kikuu MDC cha Tsvangirai.
Hata hivyo kuna masuala mengi yalio magumu.La kwanza na lililo muhimu kabisa ni iwapo Mugabe atakuwa tayari kutoa sehemu ya mamlaka yaliyomsaidia kutawala Zimbabwe kwa mabavu.Suala jingine tete ni nani atakaedhibiti majeshi ya usalama.Mugabe aliezidi kutegemea majeshi,leo katika sherehe ya kutoa heshima kwa majeshi ya taifa,aliwatunza medali majemadari 16,miongoni mwao,watatu ni marehemu.Hata kiongozi wa shirika kuu la upelelezi ametunzwa nishani.Sherehe hizo huenda zikamsaidia Mugabe wakati wa majadiliano muhimu,huku akijaribu kuwa karibu na viongozi walio na madaraka.
Lakini wanachokitaka Wazimbabwe ni makubaliano yatakayomaliza mgogoro wa kiasiasa na uchumi unaoendelea kwa takriban mwongo mmoja.Hata majirani wa Zimbabwe,wanahofia yale yatakayotokea iwapo hali itazidi kuwa mbaya nchini Zimbabwe.Kwani shida za nchi hiyo zimesababisha mamilioni ya Wazimbabwe kukimbilia nchi za ngámbo.
Wachambuzi wanasema,hali mbaya ya uchumi nchini Zimbabwe inayodhihirishwa na mfumko wa bei uliopindukia asilimia milioni 2 na upungufu mkubwa wa vyakula nchini humo ni mambo yaliyomfanya Mugabe anaetawala miaka 28 kwenda kwenye meza ya majadiliano.
Mazungumzo hayo yalianza mwezi wa Julai nchini Afrika Kusini,kufuatia machafuko yaliyozuka Zimbabwe,baada ya Mugabe kuchaguliwa rasi katika duru ya pili ya uchaguzi mwishoni mwa mwezi Juni.Uchaguzi huo ulilaaniwa kote duniani kwamba haukuwa wa haki.Vile vile ulisusiwa na Tsvangirai kwa sababu ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya wafuasi wake.
Ikiwa makubaliano ya kugawana madaraka yatapatikana kabla ya mkutano wa kilele wa SADC utakaofanywa Afrika Kusini mwishoni mwa juma,basi huo utakuwa ushindi wa kisiasa kwa mpatanishi wa majadiliano hayo Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Nchi kadhaa za magharibi zimeahidi msaada zaidi iwapo Tsvangirai na chama cha MDC watapewa dhima ya uongozi katika serikali itakayoundwa.
Mugabe anajikuta akizidi kutengwa baada ya nchi nyingi za Kiafrika na magharibi kukataa kutambua ushindi wake katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais mwishoni mwa Juni.Uchaguzi huo ulisusiwa na Tsvangirai kwa sababu ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya wafuasi wake.