Maiti zaanza kuzikwa Haiti
16 Januari 2010Waziri wa Mambo ya Ndani wa Haiti amesema idadi ya watu waliouawa katika tetemeko la ardhi nchini humo huenda ikafikia 200,000. Katika mji mkuu Port-au-Prince, wasaidizi na waokoaji kutoka zaidi ya nchi 30 wanatoa misaada ya dharura huku maiti zikiendelea kurundikwa kando ya barabara .Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa katika mji huo, hadi nusu ya majengo ama yamebomoka au yameteketezwa.
Rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi yake inafanya kila kiwezekanacho kuwasaidia wakazi wa Haiti. Wanajeshi wa majini na nchi kavu wa Marekani wamekabidhiwa dhamana ya kusimamia uwanja wa ndege mjini Port-au-Prince na wameanza kuratibu ugavi wa misaada. Idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini Haiti inatazamiwa kufikia hadi 10,000 . Baadhi yao wanatarajiwa kuwasili siku ya Jumatatu. Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anatazamiwa kwenda Haiti leo Jumamosi.