1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahujaji wachache kuhudhuria Hijja nchini Saudi Arabia

7 Julai 2020

Saudi Arabia imefungua mchakato wa kusajili mahujaji kutoka nje watakaoshiriki ibada ya Hajj ya mwaka huu,ikisema ni maelfu kadhaa tu watakaoruhusiwa kwenda kwenye ibada hiyo kutokana na janga la virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3euoA
Saudi-Arabien einsame Pilger in Mekka an der Kaaba
Picha: AFP

Kawaida ibada ya Hajj inayofanyika kila mwaka nchini Saudi Arabia katika mji wa Mekka inahudhuriwa na waumini zaidi ya milioni 2 kutoka sehemu mbali mbali za dunia,lakini mwaka huu hilo halitowezekana kutokana na mripuko wa virusi vya Corona.

Saudi Arabia imesema kwa mahujaji ambao tayari wako ndani ya taifa hilo ni 1000 tu watakaoruhusiwa kushiriki kwenye ibada hiyo ambayo mwaka jana ilihudhuriwa na waumini milioni 2.5 .

Mchakato wa kusajili mahujaji ulianza jana Jumatatu na unatarajiwa kumalizika siku ya Ijumaa ambapo wizara husika ya Saudi Arabia imeeleza kwamba raia wa nchi hiyo watakaoshiriki ibada hiyo ya siku tano ni asilimia 30 itakayobakia huku watu wa taaluma kadhaa wakizuiwa kushiriki ibada hiyo ikiwemo madaktari na maafisa usalama ambao waliwahi kuambukizwa virusi hivyo na kupona.

Idadi jumla ya raia kutoka mataifa ya nje watakaoruhusiwa kushiriki ibada hiyo ni asilimia 70 na mahujaji wote watapimwa virusi hivyo kabla ya kuwasili katika mji mtakatifu wa Mecca na watahitajika kukaa karantini nyumbani baada ya ibada hiyo kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Saudi Arabia.

Saudi-Arabien  | Hadsch Pilgertfahrt nach Mekka
Waislamu wakiswali katika msikiti mkuu mjini MeccaPicha: Reutesr/W. Ali

Hatua hii ya kuwatenga mahujaji wanaofika kutoka mataifa ya nje ya Saudia inafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo na imezusha hali ya kuvunjika moyo miongoni mwa waumini wakiislamu dunia nzima ingawa wengi wanakubali kwamba ni hatua inayohitajikakutokana na kitisho kikubwa cha kiafya kinachotajwa.

Kufikia sasa Saudi Arabia imeripoti zaidi ya visa 213,000 vya maambukizi ikiwa ni idadi kubwa kabisa katika ukanda wa nchi za Ghuba na kiasi watu 2000 wamekufa kutokana na maradhi hayo nchini humo.

Kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa cha SaudiCDC kimechapisha orodha ndefu ya maelekezo ya kuzingatiwa na mahujaji pamoja na wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuzingatiwa kwa sheria ya kukaa umbali wa mita moja na nusu kwa mahujaji ikiwemo wakati wa ibada ya swala na ibada nyingine zitakazofanywa kwenye migahawaau ndani ya mahema. Ibada ya Hajj itaanza rasmi mwisho wa mwezi huu wa Julai.

 

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW