1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Mahmoud Abbas: Israel inaendesha vita vya maangamizi Gaza

27 Desemba 2023

Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amesema mashambulizi ya Israel yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza ni "zaidi ya vita vya maangamizi" huku akiilaumu Marekani kuwa inawajibika kwa kuendelea kwa vita hivyo.

https://p.dw.com/p/4acyW
Palästinenser-Präsident Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas alipohudhuria mkutano wa dharura wa Shirika la ushirikiano la mataifa ya Kiislam (OIC) mjini Riyadh nchini Saudi Arabia:11.11.2023Picha: Saudi Press Agency/Newscom/picture alliance

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Misri, Mahmoud Abbas amesema kuwa Watu wa Palestina hawajawahi kushuhudia vita kama hivyo hata wakati wa mzozo wa mwaka 1948 unaofahamika zaidi kwa kiarabu kama Nakba ambapo maelfu ya watu walilazimika kuyahama makazi yao.

Rais huyo wa Mamlaka ya Palestina ameeleza pia kwa huzuni kuwa kila mara Ulimwengu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanapojaribu kusitisha vita hivyo, Marekani hutumia kura yake ya turufu inayozuia usitishwaji wa mapigano na kusisitiza kuwa kinachoendelea huko Gaza kinafanyika kwa msaada wa Marekani.

Soma pia: Mkuu wa jeshi la Israel anasema vita dhidi ya Hamas vitaendelea kwa miezi mingi ijayo

Eneo masikini la Ukanda wa Gaza lenye watu wapatao milioni 2.3 linahitaji makumi ya mabilioni ya dola ili kujengwa upya. Hayo ikiwa ni kwa mujibu wa Mahmoud Abbas ambaye aliuongoza ukanda huo hadi pale kundi la Hamas lilipochukua udhibiti wa eneo hilo mnamo mwaka 2007 katika kile kiongozi huyo amesema ilikuwa ni "mapinduzi."

Kauli ya Waziri Mkuu wa Palestina na wasiwasi wa Ufaransa

Addis Abeba Treffen Africa Union | Palästinensischer Ministerpräsident Mohammad Shtayyeh
Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh akihutubia katika Mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia:05.02.2021Picha: AMANUEL SILESHI/AFP

Naye Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh akiwa katika mkutano na Baraza lake la Mawaziri hii leo mjini Ramallah ameituhumu Israel kuwa inawaua watu kwa njaa huku akitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuwasilisha misaada na kutaka wahusika wa uhalifu kuhukumiwa.

"Naomba Umoja wa Mataifa ufanye kazi ya kuleta misaada kupitia vivuko vyote vitano vinavyoelekea Ukanda wa Gaza. Pia namuomba Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC aanze mara moja taratibu na hatua za kisheria kwa wale wote waliohusika na matukio ya uhalifu dhidi ya watu wetu kila mahali."

Soma pia: Israel: Mapambano dhidi yaHamas yatadumu miezi kadhaa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeelezea wasiwasi mkubwa kufuatia kauli ya Israel kwamba itazidisha na kurefusha mapigano dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza huku serikali ya mjini Paris ikisisitiza kwa nguvu zote usitishwaji mara moja wa mapigano na ikilaani mashambulio ambayo yamesababisha vifo vya raia wengi katika siku za hivi karibuni.

(Vyanzo: DPAE, AFPE, DW)