1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa kisiasa Madagascar kukutana uso kwa uso

Kabogo Grace Patricia5 Agosti 2009

Viongozi hao, Rais wa muda Andry Rajoelina na Marc Ravalomanana, wanakutana kwa mazungumzo nchini Msumbiji.

https://p.dw.com/p/J4GF
Rais wa muda wa Madagascar, Andry RajoelinaPicha: AP

Mahasimu wa kisiasa wa Madagascar wanakutana hii leo kwa mara ya kwanza mjini Maputo, Msumbiji, tangu kiongozi wa upinzani nchini humo, Andry Rajoelina alivyochukua madaraka baada ya Rais Marc Ravalomanana kuondolewa madarakani, hivyo kuchochea mkwamo wa kisiasa kwa miezi kadhaa. Ajenda kuu ya mazungumzo hayo ni kuhusu mzozo wa kisiasa katika kisiwa hicho.

Ravalomanana aliyewasili hii leo nchini Msumbiji na Rajoelina aliyewasili jana usiku, hawajazungumza na waandishi wa habari. Mahasimu hao wa kisiasa mapema leo walikutana kila mmoja kwa muda wake na mpatanishi wa mazungumzo hayo Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano, ambapo jioni hii watakuwa na mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana. Katika vikao hivyo vya awali, mahasimu hao walitaarifiwa juu ya mkutano wa leo.

Mjumbe wa timu ya wapatanishi wa Umoja wa Mataifa, Tiebele Drame, amesema kitendo cha viongozi hao wa kisiasa kukubali kuhudhuria mazungumzo hayo ni dalili njema na kupongeza hatua hiyo baada ya vikao kama hivyo kuvunjika. Drame, amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona kuwa viongozi hao wa Madagascar wanapata suluhu ya mzozo huo wa kisiasa. Mazungumzo hayo ya siku nne yatawahusisha pia marais wa zamani wa Madagascar, Didier Ratsiraka na Albert Zafy. Wanasiasa hao wanaviwakilisha vyama vinne vya kisiasa kisiwani Madagascar kilichokumbwa na mivutano ya kisiasa tangu mwezi Januari mwaka huu.

Akizungumza baada ya kuwasili nchini Msumbiji, Rajoelina amesema kuwa anataka kutafuta muafaka kwa kumaliza mzozo huo, akisema kuwa hayo yatafanyikiwa kwa kufanya kazi pamoja na viongozi watatu wa zamani wa Madagascar.

Zafy aliyeiongoza Madagascar kuanzia mwaka 1993 hadi 1996, amesisitizia umuhimu wa mazungumzo hayo akisema kuwa mzozo huo ni hatari na anatumai mazungumzo hayo yatafanikiwa kwa kupatikana suluhu. Madagascar imekuwa katika mvutano wa kisiasa tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na kutoelewana kwa Ravalomanana na Rajoelina, meya wa zamani wa Antananarivo na kiongozi wa upinzani.

Baada ya maandamano yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100 na Ravalomanana aliondolewa na jeshi lake lililoongoza nchi kabla ya kukabidhi madaraka mara moja kwa Rajoelina, huku kiongozi aliyeondolewa madarakani akiilaumu Ufaransa kuwa na mkono wake katika amatukio hayo, madai ambayo Uafaransa iliyakanusha.

Kawa upande wake Ravalomanana anayeishi uhamishoni Afriaka kusini amekua akiitembelea miji mikuu kadhaa ya nchi za kiafrika kutafuta uungaji mkono , hatua ambayo kwa sehemu ilizaa matunda baada ya umoja wa Afrika kulaani kuondolewa kwake madarakani. Tangu wakati huo, jumuiya ya kimataifa nayo ikaamua kusimamisha baadhi ya misaada yake kwa Madagascar, moja kati ya nchi masikini duniani.

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), walimteua Chissano kuwa mpatanishi wa mzozo wa Madagascar, baada ya juhudi za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kukwama.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/APE)

Mhariri:M. Abdul-Rahman