1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu Lebanon wafikia makubaliano kumaliza mvutano wa kisiasa

21 Mei 2008

Makubaliano hayo yamefikiwa leo baada ya kufanyika mazungumzo ya siku sita yaliyosimamiwa na nchi za kiarabu huko Qatar.

https://p.dw.com/p/E3eg
Hatimae maafikiano kati ya Hezoballah na serikali ya Lebanon yatangazwa QatarPicha: AP

Hatua hiyo mpya sasa inafungua njia kwa bunge kumchagua mkuu wa majeshi Michel Suleiman kuwa rais wa Lebanon nafasi ambayo imekuwa wazi tangu mwezi Novemba baada ya kumaliza kipindi chake madarakani rais Emile Lahoud.Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa hii leo mkuu wa majeshi Michel Suleiman anatazamiwa kuchaguliwa na bunge kuwa rais mpya wa Lebanon katika kipindi cha saa 24.Spika wa bunge Nabih Berri amesema kulingana na makubaliano kati ya viongozi wa kisiasa inabidi Suleiman achaguliwe rais wiki hii.Maafikiano kati ya kundi la Hezbollah na serikali ya mseto ya Lebanon inayoungwa mkono na Marekani yamefikisha mwisho mvutano juu ya sheria ya bunge ya uchaguzi na pia kuzingatia mapendekezo ya muda mrefu ya upande wa upinzani yaani Hezbollah ya kutaka kuwa na kura ya turufu serikalini.Makubaliano hayo pia yametilia mkazo pande zote mbili serikali na upinzani kuachana na matumizi ya nguvu katika mivutano ya kisiasa.Tareq Mitri ni kaimu waziri wa mambo ya nje wa Lebanon amesema Makubaliano haya ni mfano bora kwa walebanon kuelewa kwamba wanahitaji kuwa na makubaliano kwa njia inayofaa,kwamba wayatatue matatizo yao kwa kuelewana na kuzingatia uhalali wa malalamiko yanayohusu vyama vyote lakini pia wakati huohuo tuheshimu mfumo wa demokrasia uliopo na ambao utaendelea kuwepo Lebanon.''

Waziri mkuu wa nchi hiyo Fuad Siniora kwa upande wake akizungumza katika sherehe hiyo ya kusainiwa makubaliano amesema walebanon hawana budi kuwa na mshikamo ili kuwa na mustakabala mwema wa nchi yao.

Kundi la Hezbollah likiungwa mkono na Iran na Syria liliongeza shinikizo dhidi ya chama tawala mapema mwezi huu kwa kuwaongoza wafuasi wake katika kamepini ya kijeshi.Katika ghasia za hivi karibuni nchini Lebanon watu 81 waliuwawa na wengine wengi wakajeruhiwa.Ghasia hizo ndio mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1^975 hadi 1990.

Serikali ya Lebaon kwa muda mrefu imekuwa ikipinga mapendekezo ya upinzani ambao unaungwa mkono na Syria ya kutaka kura ya turufu katika maamuzi ya serikalini ikisema kwamba Hezbolah linajaribu kurudisha ushawishi wa Syria kudhibiti Lebanon.Itakumbukwa kwamba Syria ililazimika kuondoa wanajeshi wake nchini Lebanon mwaka 2005 baada ya kuuwawa kwa waziri mkuu wa zamani Rafiq Hariri.Aidha mawaziri kutoka kundi la Hezbollah walijiuzulu serikalini mwezi Novemba mwaka 2006 kuipinga serikali baada ya kukataa matakwa ya Hezbollah ya kutaka kuwa na kura ya turufu katika maamuzi ya serikali.

►◄