Mahakimu wajitoa kusikiliza kesi Misri
29 Februari 2012Duru za mahakama zimearifu kwamba mahakimu hao waliamua kuacha kuzisikiliza kesi zinazowakabili wanaharakati wanaotetea demokrasia nchini Misri. Wanaharakati hao ni pamoja na Wamarekani.
Kesi za watu hao zilianza kusikilizwa huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton aliwaambia Maseneta kwamba utawala wa Obama unafanya mazungumzo na Misri kwa matumaini ya kufikia suluhisho la haraka. Marekani inataka Wamarekani hao 19 wanaobalikiwa na kesi nchini Misri waachiwe.
Jumla ya wanaharakati 43 wanakabiliwa na kesi ikiwa pamoja na Wamarekani hao, na wengine kutoka nchi nyingine. Lakini hakuna alietokea mahakamani jumapili iliyopita. Kwa mujibu wa taarifa, wanaharakati hao wa Marekani wanajihifadhi kwenye ubalozi wa nchi yao mjini Cairo.
Bado haijakuwa wazi iwapo uamuzi wa mahakimu wa Misri kujitoa katika kuzisikiliza kesi hizo umetokana na shinikizo la Marekani. Hata hivyo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Clinton amearifu kwamba mazungumzo ya ndani yanafanyika na wahusika wa Misri juu ya kesi zinazowakabili raia wao 19.
Wanaharakati wa Misri wa mashirika yasiyo ya kiserikali wanakabiliwa na mashtaka ya kupokea fedha kutoka nje kinyume cha sheria na kwa kufanya kazi bila ya kibali. Shirika la habari la AFP limearifu kwamba washtakiwa 14 ambao hawakutokea mahakamani jumapili iliyopita wameyakanusha mashtaka yanayowakabili.
Bila ya maelezo yoyote mahakimu waliokuwa wanasikiliza kesi za wanaharakati hao waliamua kujitoa. Lakini Shirika la habari la Misri MENA limesema Hakimu Mkuu Mohammed Shukry aliandika barua kwa Mkuu wa mahakama ya rufani kusema kwamba yeye na mahakimu wenzake hawataweza tena kuendelea kuzisikiliza kesi zinazowakabili wanaharakati. Shirika la MENA limekariri msemo unaoweza kuwa na maana ya kutojisikia vizuri katika kuzisilikiza kesi hizo au maana ya kukabiliwa na vizingiti katika kazi zao.
Kesi zinazowakabili wanaharakati zinafuatia kuvamiwa kwa ofisi kadhaa za asasi ambazo siyo za kiserikali mjini Cairo mnamo mwezi wa Desemba Wanaharakati wa kimarekeni wanakabiliwa na tuhuma za kuwapa mafunzo wanaharakati wa Misri juu ya kuendesha kampeni za uchaguzi wa bunge.
Kesi za wanaharakati hao ikiwa pamoja na wa kutoka Marekani zimesababisha mkwaruzano katika uhusiano baina ya Misri na Marekani.
Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/
Mhariri/ Abdul-Rahman.