Mahakama ya Pakistan: Kukamatwa kwa Khan ni 'batili'
11 Mei 2023Kitendo cha kukamatwa Imran Khan mapema wiki hii, kilisababisha kuzuka kwa ghasia za wenyewe kwa wenyewe nchini Pakistan. Jaji Mkuu wa Pakistan, Umar Ata Bandial amemwambia Khan kwamba kukamatwa kwake ni ''batili'', hivyo mchakato mzima unahitaji kuangaliwa upya. Jopo la majaji watatu liliombwa kusikiliza ombi la Khan katika Mahakama ya Islamabad kupinga kukamatwa kwake siku ya Jumanne kwa tuhuma za ufisadi.
Huku wakiamuru kuachiwa kwa Khan kutoka rumande, mahakama hiyo imemtaka waziri huyo mkuu wa zamani kushirikiana na Ofisi ya Kitaifa ya Uwajibikaji, ambayo inachunguza mashataka dhidi yake.
Khan atakiwa kulaani ghasia
Jaji Bandial pia amemtaka Khan, mwenye umri wa miaka 71 kulaani maandamano ya ghasia ambayo yamezuka baada ya kukamatwa kwake. Wafuasi wa Khan walionekana wakicheza karibu na jengo la mahakama kushangilia uamuzi huo wa mahakama.
Mkuu wa timu ya mawakili wa Khan, Babar Awan amewaambia waandishi habari kwamba ingawa mteja wao ameachiwa huru kutoka kizuizini, ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa vikosi vya usalama katika eneo salama kwenye mji mkuu, Islamabad. Awan amesema Khan atafikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Pakistan siku ya Ijumaa.
Khan amesema kesi kadhaa za kisheria zilizowasilishwa dhidi yake, ni sehemu ya juhudi za serikali na jeshi kumzuia kurejea madarakani kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika wakati wa majira ya mapukutiko. Awali jeshi lilionya kuhusu kuchukua hatua kali kwa mashambulizi yoyote yale dhidi ya majengo ya serikali na jeshi na kwamba lawama zitabebeshwa kwa kundi ambalo linataka kuitumbukiza Pakistan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Jeshi lapelekwa Punjab na Islamabad
Siku ya Jumatano, serikali iliidhinisha kupelekwa kwa jeshi katika majimbo mawili ikiwemo la Punjab, lenye watu wengi zaidi na kwenye mji mkuu, Islamabad kwa ajili ya kurejesha amani. Serikali imekuwa ikiwakandamiza wafuasi wa Khan na imewakamata zaidi ya watu 20,000 katika misako tofauti nchi nzima.
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amevitaka vikosi vya usalama vya Pakistan kujizuia na amesema waandamanaji wanapaswa kujizuia na ghasia. Turk ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa uhuru wa kujielezea, kukusanyika kwa amani na utawala wa sheria ni muhimu katika kusuluhisha mizozo ya kisiasa bila kutumia nguvu zisizo na uwiano.
(AFP, AP, DPA, Reuters)