1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Kenya yaamuru mali ya Kabuga kuendelea kuzuiliwa

28 Aprili 2023

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kuwa mali ya bilionea na mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994, Felicien Kabuga, itaendelea kuzuiliwa hadi pale korti ya Umoja wa Mataifa itakapohitimisha kesi.

https://p.dw.com/p/4QfSe
Ruanda Der Geschäftsmann Felicien Kabuga
Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Hapo jana Alhamisi, Jaji Esther Maina amelikataa ombi la familia ya Kabuga la kufutilia mbali amri ya kuzuwia mali ambayo ni nyumba ya mtuhumiwa iliyoko jijini Nairobi.

Mali hiyo inazuiliwa baada ya mwanasheria mkuu kuamuru hilo ili kutimiza azimio linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa ushirikiano katika kesi zinazowahusu watuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda.

Kabla ya kifo chake, marehemu mkewe Kabuga, Mukazitoni Josephine, aliiambia mahakama kuwa hakuna ushahidi kwamba mali hiyo ilipatikana kinyemela au mapato yake ya kodi kutumika kuzuwia kukamatwa na pia kuwavuruga mashahidi.

Felicien Kabuga alikamatwa mwezi Mei 2020  nje kidogo ya mji wa Paris na anazuiliwa kwenye mahakama ya uhalifu wa kivita ya The Hague kwa mashtaka yanayohusiana na mauaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994.