Marufuku ya kusafiri ya Trump kuanza kutekelezwa
5 Desemba 2017Hatua hiyo inafuatia mahakama ya juu nchini humo kubatilisha mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa na mahakama za chini ambayo kwa kiasi fulani yalizuia utekelezaji wake.
Amri hiyo ilikua imewekewa pingamizi na wanasheria wa haki za binadamu kuwa ni marufuku dhidi ya Waislamu na kuwa inakiuka katiba ya Marekani na haikua na uthibitisho wa kutosha kuhusiana na hatari ya usalama kama ambavyo serikali imekua inadai.
Marufuku hiyo ya muda inayalenga mataifa ya Iran, Libya, Syria, Yemen, Somalia na Chad huku Korea Kaskazini na baadhi ya maafisa kutoka Venezuela wakiongezwa katika orodha ya sasa.
Trump bado ameendelea kusisitiza kua marufuku hiyo ni kwa ajili ya kulinda usalama wa Marekani.
Amri hiyo ya Trump ilikosolewa huku baadhi ya mahakama nchini Marekani zikiamua kuwa Trump hawezi kuwazuia walio na uhusiano na watu nchini Marekani kutoingia nchini humo.
Watu walioweka pingamizi dhidi ya amri hiyo walishawishi mahakama kusitisha utekelezaji wake wakati wao na wanasheria wa serikali wakitafuta uhalali kisheria kuhusiana na marufuku hiyo.
Hata hivyo, utawala wa Trump ambao unasema marufuku hiyo ni muhimu ili kuilinda Marekani na kuzuia mashambulizi ya kigaidi pamoja na usalama wa nchi hiyo kwa ujumla imepata uungwaji mkono mkubwa katika mahakama ya juu ambapo majaji saba dhidi ya wawili wameunga mkono marufuku hiyo iendelee wakati rufaa ikisubiriwa.
Ikulu ya Marekani yasema haishangazwi na uamuzi wa mahakama
Taarifa ya ikulu ya Marekani-White House, imesema hawashangazwi na uamuzi wa mahakama ya juu wa kuruhusu mara moja kuendelea kwa utekelezaji wa marufuku hiyo ya rais inayolenga nchi zinazohusishwa zaidi na masuala ya ugaidi.
Baraza linalohusika na masuala ya uhusiano wa nchi za Kiislamu na Marekani ambalo ni shirika kubwa zaidi la kupigania haki za kiraia za waislamu limekosoa uamuzi huo wa sasa.
Majaji wa mahakama ya juu wamesema wanatarajia mahakama za rufaa za chini kuharakisha uamuzi wao ili kutoa nafasi iwapo kutakua na uwezekano suala hilo kurejeshwa mahakama ya juu likiwa ni pingamizi lingine la kisheria dhidi ya ikulu ya Marekani.
Mahakama ya San Francisco inatarajia kusikiliza kesi hiyo Jumatano na mahakama ya Richmond itafanya hivyo Ijumaa.
Trump alitangaza kwa mara ya kwanza marufuku ya kusafiri baada ya kuingia rasmi madarakani Januari mwaka huu. Hata hivyo baada ya marufuku ya awali iliyohusisha mataifa sita muda wake kumalizika Septemba , utawala wa rais Donald Trump ulitangaza marufuku nyingine na safari hii Chad ikiongezwa katika orodha wakati Sudan iliondolewa huku Korea Kaskazini na Venezuela zikiongezwa pia.
Idara inayohusika na masuala ya uhamiaji pamoja na wanaharakati wanaopigania haki za kiraia wanasisitiza kwamba marufuku hiyo kimsingi bado inawalenga waislamu na inakikuka katiba ya Marekani kuhusiana na uhuru wa dini.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo