Mahakama India yaondoa mfumo usio wazi wa ufadhili kisiasa
15 Februari 2024Mahakama imesema mfumo huo unakwenda kinyume cha sheria. Uamuzi huo umeonekana kama pigo kwa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi cha Bharatiya Janata, ambacho kimekuwa mnufaika mkubwa zaidi wa mfumo huo ulioanzishwa mwaka wa 2017.
Mfumo huo unaoitwa Dhamana za Uchaguzi, ulipingwa na wanachama wa upinzani na asasi za kiraia kwa madai kuwa unazuia haki ya umma kujua nani ametoa fedha kwa vyama vya siasa.
Chini ya mfumo huo, mtu au kampuni ingeweza kununua hati za dhamana kutoka Benki ya Taifa ya India na kutoa kama mchango kwa chama cha kisiasa.
Soma pia:Polisi wamwagwa India kuwakabili wakulima wasiandamane
Mahakama hiyo yenye majaji watano ikiongozwa na Jaji Mkuu D. Y. Chandrachud imesema michango ya kisiasa inampa mchangiaji nafasi ya ushawishi katika masuala ya kutunga sera.