1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya EAC yatupilia mbali kesi ya upinzani TZ

17 Juni 2020

Mahakama ya Afrika Mashariki imetupilia mbali ombi la zuio la muda lililopelekwa na vyama vya upinzani la kusitishwa utekelezwaji wa sheria ya vyama vya siasa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/3dufL
Tansania: Online Gerichtsverhandlung in Shinyanga
Picha: DW/V. Natalis

Upinzani uliwasilisha kesi hiyo kwa madai kuwa baadhi ya vipengele katika sheria hiyo vinaminya uhuru wa demokrasia kwa vyama hivyo

"Sheria ya vyama vya siasa ya Tanzania iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ni halali, vyama vya siasa viendelee kuiheshimu mpaka pale mahakama hii itakaposikiliza kesi ya msingi ya kutengua maamuzi hayo,” alisema Jaji kiongozi Audace Ndiye.

Mahakama hiyo imeamua kuwa sheria hiyo itatumika kama ilivyo, huku shauri la msingi likiendelea kusikilizwa.

Viongozi wa upinzani walifungua kesi dhidi ya mwanasheria mkuu wa Tanzania

Freeman Mbowe mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Chama cha ACT Wazalendo, chama cha Chauma na aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwa pamoja walifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali, kupinga baadhi ya vipengele vilivyo katika sheria ya vyama vya siasa nchini Tanzania, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Tansania Daressalam Maalim Seif Shariff Hamad und Freeman Mbowe im gericht
Maalim Seif (kushoto) na Freeman Mbowe (kulia)Picha: DW/S. Khamis

Baadhi ya vipengele vinavyopingwa ni pamoja na kile kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kuingilia michakato ya kisiasa ndani ya vyama vya siasa, kuzuia ulinzi binafsi kwa vyama vya siasa na wanasiasa pamoja na kuzuia mashirika ya kiraia na watu binafsi kutoa mafunzo kwa vyama vya siasa pasipo idhini ya msajili wa vyama vya siasa. Baada ya mahakama hiyo kukataa ombi la vyama vya upinzani kuzuia kwa muda utekelezwaji wa sheria hiyo, wakili Jebra Kambole anayesimamia kesi hiyo amesema watakata rufaa haraka.

Mahaka hiyo pamoja na kukiri kuwa hoja ya vyama vya upinzani ni ya msingi, lakini imeona kuwa ombi hilo la zuio la muda linatupiliwa mbali kwa sababu hakuna madhara makubwa yatawapata ambayo hayawezi kufidiwa kwa pesa au kwa namna nyingine yoyote, na kwamba kesi ya msingi ya kupinga sheria hiyo itaendelea kusikilizwa.

Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inatajwa kukiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na haki nyingine za binadamu.