Mahakama ya EAC yasikiliza kesi ya vyama vya siasa Tanzania
19 Juni 2019Mahakama ya sheria ya Jumuiya ya Afrika mashariki iliyopo makao makuu ya jumuiya hiyo katika mkoa wa Arusha kaskazini mwa Tanzania, leo imetoa maamuzi kuhusu maombi ya vyama vya upinzania nchini Tanzania madai yaliyokuwa yanahitaji kusikilizwa kwa hati ya dharura na kwa upande mmoja kuhusu kupinga sheria ya vyama vya siasa ambapo mahakama hiyo imesema lazima upande wa serikali ambao ni walalamikiwa upate nafasi ya kusikilizwa.
Katika kesi hiyo kiongozi wa jopo la mawakili wanaowakilisha vyama vya upinzani wakili Fatuma Karume, aliiambia mahakama hiyo mbele ya jaji kiongozi Monica Mugenyi kwamba upande wa upinzani unaiomba mahakama izuie kwa muda utekelezaji wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya sisa ya mwaka 2019.
Katika sheria hiyo vifungu vinavyobishaniwa ni kifungu cha 5A kinachozuia mtu au taasisi yeyote kutoa elimu ya uraia bila idhini ya msajili wa vyama vya siasa.
Mahakama hiyo imesema ni lazima walalamikiwa ambao ni serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania wapate nafasi ya kusikilizwa ili kuzingatia suala la haki.
Sheria hiyo inaelekeza kwamba kana mtu au taasisi yeyote inataka kutoa elimu ya uraia iombe kibali kwa msajili wa vyama vya siasa siku 30 kabla, ikionesha vitendea kazi vinavyokwenda kutumika, sababu za kutoa elimu hiyo, watu wanaokwenda kupatiwa elimu pamoja na matokeo yatakayopatikana baada ya elimu hiyo kitu ambacho vyama vya upinzani vionaona ni ukiukwaji wa mkataba wa jumuiya ya Africa mashariki ibara ya sita ambayo insisitiza uwepo wa demokrasia.
Maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura yaananza kufanyika katika kanda ya kaskazini hasa kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha tarehe 23 mwezi huu wa june, na kwa sheria hiyo vyama vya upinzania vinasema haviwezi kuapata nafasi ya kutosha kuwaelimisha wananchi kuhusu uborehwaji wa daftrari la kudumu la wapiga kura.
Kesi hiyo iliyopelekwa kwa hati ya dharura na kuombwa kusikilizwa kwa upande mmmoja imezua mvutano baina ya walalamikaji na jaji anayesikiliza kesi hiyo akihoji kama ni haki mahaka hiyo ya Afrika mashariki kusikiliza kesi hiyo kwa hati ya dharura na kwa upande mmoja ambapo wakili Fatuma Karume ambaye ni kiongozi wa jopo la mawakili wanaowakilisha vyama vya upinzani ameiambia mahakama hiyo kuwa walalamikiwa ambao ni serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania walikuwa na taarifa tangu mwezi April mwaka huu na zoezi la uandikishwaji wa wapiga kura ni la haraka.