1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama kuu ya Venezuela yabatilisha uamuzi wake wa awali

2 Aprili 2017

 Mahakama kuu nchini Venezuela imeghairi uamuzi wake juu ya kutwaa mamlaka ya bunge linalodhibitiwa na upinzani.  Uamuzi huo ulisababisha shutuma kutoka duniani kote. Maandamano makubwa yalifanyika nchini Venezuela.

https://p.dw.com/p/2aVdY
Venezuela Anti Regierungsproteste
Picha: Reuters/M. Bello

Mahakama hiyo kuu ilisema katika uamuzi uliochapishwa kwenye tovuti yake kwamba imeibatilisha hukumu iliyoitoa tarehe 29 mwezi Machi juu ya kulinyng'anya bunge mamlaka, baada ya hukumu hiyo kusababisha wasiwasi kwamba Venezuela inaelekea kwenye udikteta chini ya rais wa mrengo wa shoto Nicolas Maduro.  Mahakama hiyo pia imeghairi uamuzi wake wa kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria.

Hatua hiyo mpya imechukuliwa na mahakama kuu baada ya rais Nicolas Maduro kuitaka taasisi hiyo iupitie upya uamuzi wake na pia baada ya kufanyika mkutano juu ya usalama wa nchi hapo jana. Wapinzani na mkuu wa shirika la nchi za Amerika waliufananisha uamuzi wa mahakama kuu na kutwaa mamlaka kwa nguvu.  Uamuzi wa mahakama hiyo inayoegemea upande wa rais Maduro ulishutumiwa pia na Marekani, Umoja wa Ulaya, Brazil, Mexico , Argentina, Chile na Colombia.

Venezuelas Präsident Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduraPicha: picture-alliance/dpa/A. Rivera/P. Miraflores

Uamuzi wa mahakama kuu wa jana ulionyesha mgeuko usio wa kawaida kwa rais Madura, Msoshalisti ambaye alionekana kuvuka mipaka katika njama zake za kutaka kuyaimarisha mamlaka yake.  Hata mwanasheria mkuu wa Venezuela Luisa Ortega, ambaye ni mshirika wa Maduro alipinga hatua ya kulinyag'anya bunge mamlaka. Ortega alieleza kuwa hatua hiyo ilikiuka taratibu za katiba.

Viongozi wa upinzani wamesema uamuzi wa mahakama kuu wa kughairi hukumu yake ni ushuhuda kwamba mfumo wa sheria unadhibitiwa na rais Maduro.  Kiongozi wa bunge Julio Borges amesema huwezi kujifanya unarejesha hali ya kawaida nchini baada ya kufanya mapinduzi.  Hapo awali bwana Borges aliichana hati ya uamuzi wa mahakama kuu kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Katika uamuzi wake wa siku ya Jumatano mahakama kuu ya Venezuela ilisema wabunge waliidharau mahakama kwa kukataa kuyazingatia maamuzi ya hapo awali yaliyobatilisha sheria iliyopitishwa na bunge.

Mahakama hiyo kuu ya nchini Venezuela imetengua maamuzi kadhaa ya bunge na kulivua mamlaka  tangu wapinzani washinde uchaguzi uliofanyika mwaka 2015. Juhudi za mara kwa mara za wapinzani za kutaka kufanyika kura ya maoni na uchaguzi mpya kabla ya kumalizika kwa muhula wa rais Maduro zimekuwa zinapingwa na mahakama hiyo kuu pamoja na tume ya uchaguzi.  Muhula wa rais Maduro unamalizika mwaka 2019.

Kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja rais huyo amekuwa anaongoza kwa amri za dharura ili kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi ambao umesababisha wasiwasi kwamba huenda Venezuela ikasambaratika na hivyo kusababisha hali mbaya ya kiusalama na maafa kwa binadamu katika kanda ya Amerika.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/ dw.com/p/2aUr8

Mhariri: Sudi Mnette