Mahakama Kuu ya Ujerumani yaamua wakimbizi wapewe fedha zaidi
18 Julai 2012Huyo ni Makamo wa Rais wa Mahakama Kuu ya Ujerumani, Ferdinand Kirchhof, akisoma hukumu inayowapa sasa waombaji 13,000 wa hifadhi nchini Ujerumani ongezeko la zaidi ya euro 100 kwenye fedha za kujikimu. Kwa uamuzi huo, sasa kila muombaji hifadhi aliyefikia umri wa mtu mzima atapokea euro 336 kutoka zile 240 alizokuwa akipokea hapo mwanzoni.
"Baraza la Senate la Mahakama limeamua kwamba fedha zinazotolewa chini ya Sheria ya Mafao kwa Wanaoomba Hifadhi hazitoshi kukimu mahitaji ya chini ya msingi kwa mwanaadamu kwa mujibu wa Katiba. Bunge linapaswa kuipitia upya na kufanya marekebisho yanayohitajika." Amesema Jaji Kirchhof wakati akisoma hukumu hivi leo.
Katika hukumu ya leo, mahakama hiyo pia imesema kwamba imegundua kwamba kiwango cha fedha kinachotolewa kwa watu wanaosubiri majibu ya maombi yao ya hifadhi hakipigiwi hisabu vyema na wala si halisi, na hivyo kuamuru kwamba kwa sasa, wakati serikali ikirekebisha sheria hiyo ya mafao, iwalipe waombaji hifadhi kama inavyowalipa raia wasiokuwa na kazi, ambao hupokea euro 374 kwa mwezi
Wakimbizi wapewe haki kama wengine
Mahakama Kuu imeona licha ya kuwa tayari waombaji hifadhi huwa wameshapatiwa nyumba na huduma za afya bure, bado kiwango cha awali cha fedha, ambacho kimekuwa kikitumika tangu mwaka 1993, kilikuwa hakiwawezeshi kujikimu kimaisha.
Hili, hata hivyo, haliyafanyi maisha ya wakimbizi nchini Ujerumani kuwa bora. Festus Tanwi, mmoja wa vijana wa Cameroon wanaoomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani, anasema kwamba wanadhalilika sana.
"Unaishi kwenye chumba kimoja na pengine hutaki kuweka wazi mambo yako ya faragha, unapaswa kuvua nguo mbele ya mtu ambaye hamutoki familia wala hata nchi moja. Huna heshima yoyote katika maisha yao. Huna faragha yoyote."
Pamoja na kurundikwa katika nyumba zisizokidhi viwango, wakimbizi na wageni nchini Ujerumani hukabiliwa pia na ubaguzi wa wazi kutoka kwa wenyeji.
"Sisi pia ni wanaadamu kama wao. Tunavuta hewa kama wao. Tuna damu nyekundu pia. Hivyo sifahamu kwa nini wanatukatalia haki yetu. Lakini ukweli ni kuwa tunachukuliwa kama si wanaadamu kamili." Anasema Tony Maimba, mkimbizi kutoka Kenya.
Mwaka jana, Ujerumani iliwachukua watu 13,000 wanaoomba hifadhi ya ukimbizi na kuifanya kuwa ya pili kwenye Umoja wa Ulaya kwa kuwa na wakimbizi wengi, ikitanguliwa na Uingereza yenye wakimbizi 14,400, kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Takwimu ya Ulaya, Eurostat.
Hata hivyo, hicho kinatajwa kuwa kiwango kidogo kulinganisha na wale wanaopigania kuingia barani Ulaya hasa kutoka Afrika na Asia, baada ya kuimarishwa kwa sheria za usafiri wa anga na Umoja wa Ulaya kuwalazimisha wakimbizi kuomba hifadhi katika nchi ya mwanzo wanayoingia barani Ulaya.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman