1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama kutoa hukumu katika kesi ya mashambulio ya Madrid ya mwaka 2004

31 Oktoba 2007

Mahakama ya mjini Madrid nchini Uhispania leo inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi ya mashambulio ya bomu dhidi ya treni nne yaliyotokea mwaka 2004 ambayo zaidi ya watu 190 waliuwawa.

https://p.dw.com/p/C77M
Mmoja kati ya washtakiwa waliofikishwa mahakamani nchini Uhispania
Mmoja kati ya washtakiwa waliofikishwa mahakamani nchini UhispaniaPicha: AP

Hali ya usalama imeimarishwa katika eneo la mahakama mjini Madrid huku uamuzi ukisubiriwa kwa hamu kutokana na mashambulio ya bomu dhidi ya treni nne nchini Uhispania yaliyotokea mwezi Machi mwaka 2004.

Mashambulio hayo ya kigaidi ni mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Uhispania.

Jopo la majaji watatu litatoa hukumu wakati wowote kuanzia sasa.

Jaiji mkuu Javier Gomez Bermudez tayari amekabishi kopi ya stakabadhi za hukumu kwa mkuu wa maslahi ya umma.

Mwendesha mashtaka mkuu Javier Zaragoza anaamini kwamba pana ushahidi wa kutosha wa kuwezesha kutoelwa adhabu.

Washtakiwa 28 wamefikishwa mbele ya mahakama wakikabiliwa na tuhuma za kufanya mashambulio dhidi ya treni nne yaliyosababisha vifo vya watu 191.

Zaidi ya watu 1500 walijeruhiwa katika mashambulio hayo.

Washtakiwa hao, 27 wanaume na mwanamke mmoja wamekanusha mashtaka dhidi yao katika muda wote wa miezi minne wakati kesi ilipokuwa inasikilizwa.

19 kati ya watuhumiwa hao 28 ni raia wa Morroco au wana nasaba za Kiarabu na tisa ni raia wa Uhispania wote wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, udanganyifu pamoja na kushiriki katika njama za mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11,mwezi Machi mwaka 2004.

Washukiwa wanane wanakabiliwa na dhabu ya kifungo cha hadi miaka elfu 39 iwapo watapatikana na hatia ya katika mashtaka yote dhidi yao.

Lakini chini ya sheria za Uhispania kifungo cha hadi miaka 40 kinatolewa kwa makosa ya ugaidi.

Raia wengi wa Uhispania bado wana shakashaka kuhusu nani hasa aliyehusika na mashambulio hayo na wengi wao pia wana amini kuwa hukumu ya leo itasaidia kufuta shaka hizo.

Waziri mkuu wa Uhispania Jose Rodriguez Zapatero amesema anataraji kwamba hukumu ya leo itatoa jibu kwa wale waliokuwa na mashaka tangu mashambulio ya tarehe 11 mwezi Machi mwaka 2004 yalipotokea.

Ni dhahiri kwamba mahakimu watasikiliza matakwa ya waendesha mashtaka.

Kesi hii iliyochukuwa muda mrefu yumkini itamalizika kwa kutolewa adhabu ndefu lakini kovu litaendelea kuwepo kutokana na mashambulio ya magaidi ya tarehe 11 mwezi Machi miaka mitatu iliyopita.

Wapelelezi wa Uhispania wanasema kuwa watuhumiwa hao walikuwa ni wanachma wa kundi la kiislamu lenye mtazamo mkali lililokuwa linafuata maadili ya kundi la kigaidi la Al Qaeda ijapo kuwa hawakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kundi hilo la kigaidi.

Wakati kesi ilipokuwa inaendelea kusikilizwa watuhumiwa 14 walisusia kula chakula kwa madai kwamba tuhuma dhidi yao hazikuwa za haki.

Watuhumiwa saba walijiuwa kwa kujilipua ndani ya nyumba moja mjini Madrid wiki tatu baada ya mashambulio hayo ya Machi 11 mwaka 2004.