Mahakama Kenya yatoa uamuzi kuhusu mashoga
23 Machi 2018Shirika linalotetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya, NGLHRC lilipeleka kesi hiyo mahakamani baada ya wanaume wawili kukamatwa mwaka 2015 kwa kuhisiwa kwamba wanashiriki mapenzi ya jinsia moja.
Wakati wa kusikilizwa kwa hukumu hiyo kwenye mji wa Mombasa, Jaji Alnashir Visram alisema kuwa uamuzi uliotolewa awali na mahakama kuu haukuzingatia katiba na ulikiuka haki za binaadamu. Mwaka 2016 mahakama moja ya Kenya ilitoa uamuzi kuwa vipimo kama hivyo vilikuwa halali kwa mujibu wa katiba.
Uamuzi wa mahakama wapongezwa
Eric Gitari, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo amesema uamuzi huo ni hatua kubwa sio tu kwa kuheshimu uhuru wa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ambao wamekuwa wakilazimika kupimwa kwa nguvu sehemu zao za kutolea haja kubwa, bali pia kwa utawala wa sheria nchini Kenya.
Amesema upimaji huo ni kinyume na haki zao za faragha za mashoga na wasagaji na heshima zao za kiutu na pia zinaweza kuchukuliwa kama kufanyiwa mateso.
Shirika hilo lilikuwa likiwawakilisha wanaume hao ambao walilazimishwa kupimwa sehemu zao za kutolea haja kubwa chini ya usimamizi wa watumishi wa hospitali na maafisa usalama. Aidha, wanaume hao walilazimishwa pia kupimwa virusi vya Ukimwi.
Shirika la NGLHRC limefafanua kuwa vipimo hivyo vinajumuisha kuwalazimisha wanaume kujilaza huku miguu yao ikiwa imenyanyuliwa juu katika hali ya kudhalilisha na kisha vifaa vinaingizwa katika sehemu zao za kutolea haja kubwa. Shirika hilo limesema vipimo hivyo haviendani na misingi ya matibabu.
Kabla ya hukumu hiyo iliyotolewa jana, Kenya ilikuwa miongoni mwa mataifa manane yanayoruhusu wanaume kupimwa kwa lazima katika sehemu zao za siri kubaini iwapo wanashiriki mapenzi ya jinsia moja, tangu mwaka 2010.
Nchi nyingine
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch, nchi nyingine ni Cameroon, Misri, Lebanon, Tunisia, Turkmenistan, Uganda na Zambia.
Gitari anasema hukumu hiyo bila shaka huenda ikaleta athari katika mataifa hayo yanayoendeleza vipimo hivyo vya lazima. Nchini Kenya kushiriki mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 gerezani.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, ILGA limeiweka Kenya katika orodha yake ya nchi ambazo zinaeneza chuki dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kupitia sera yake ya sheria za kitaifa.
NGLHRC pia imeipinga sheria ya Kenya inayowalenga watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kuvifanya vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria kuwa ni uhalifu. Aprili 26, mahakama inatarajia kutangaza tarehe ambayo itatoa uamuzi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters, DW https://bit.ly/2DNu0ag
Mhariri: Josephat Charo