1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli aeleza dira ya maendeleo ya miaka mitano ijayo

Deo Kaji Makomba
13 Novemba 2020

Rais John Pombe Magufuli amelihutubia bunge mjini Dodoma na kutishia kuwachukulia hatua kali wale wote watakaojaribu kuvuruga amani ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3lF5M
Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Kwa hotuba hiyo Rais Magufuli anaanza rasmi muhula wa pili wa Urais baada ya kushinda uchaguzi uliopita. 

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ameitoa hii leo mjini Dodoma wakati akilihutubia bunge la taifa huku akielezea dira ya maendeleo ya miaka mitano mara baada ya kuchaguliwa kuwa rais kwa muhula wa pili.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa muda wa saa moja na dakika 22 Rais Magufuli ameyataja mambo muhimu ambayo serikali yake itayafanyia kazi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa pamoja na kulinda na kudumisha tunu za taifa.

“Jambo la kwanza na muhimu tutakalolipa kipau mbele kikubwa kwenye miaka mitano ijayo ni kuendelea kulinda na kudumisha tunu za taifa letu yaani amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi yetu, muungano na mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Na katika hilo naahidi kushirikiana kwa karibu sana na Rais mpya wa Zanzibar mheshimiwa Dr. Hussein Mwinyi, kamwe hatutakuwa na mzaha na yoyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu” amesema Rais Magufuli.

Magufuli awatolea wito Watanzania kuweka katika biashara mbalimbali

Tansania Geschäftsgebiet in Dar es Salaam
Wafanyabiashara mjini Dar es SalaamPicha: DW/E. Boniphace

Aidha Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwekeza katika biashara mbalimbali na kwamba wakati wa kufanya mambo bila woga ni sasa, na pia amewatolea wito wawekezaji kutoka nje ya nchi, akisema Tanzania ni mahali salama kwa mitaji yao.

Ama kuhusiana na suala la demokrasia nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema kuwa demokrasia ni kuleta maendeleo na sio fujo na kuongeza kuwa.

“Hakuna demokrasia isiyo na mipaka, aidha uhuru na haki vinakwenda sambamba na wajibu na hakuna uhuru au haki isiyokuwa na wajibu. Vyote vinakwenda sambamba. Najua nimeelewaka vizuri. Mheshimiwa spika, kama nilivyoahidi wakati wa kipindi cha kampeini kwenye miaka mitano ijayo tutaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo” amesema Rais Magufuli katika hotuba yake bungeni hii leo.

Hotuba hiyo ya Rais Magufuli imepokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara nchini Tanzania. Al Tafu Mansoor Dogo ni miongoni mwa wafanyabiashara kutoka Mwanza.

"Nimeona amesema kwamba  vijana wa boda boda, mama ntilie, machinga,.Hawa wote ni nguvu kazi yetu na hawa pia wana haki wapewe fursa ya kuwa wafanyabiashara wakubwa. Hiyo inatia Imani na kusema, hapana kila mmoja anayefanya biashara ambaye ni mdogo atapewa fursa ya kuwa mfanyabiashara mkubwa na mwisho wa siku awe bilionea pia. Hii ni nchi yetu."

Hatua ya Rais Magufuli kulihutubia bunge la 12 la Tanzania, imekwenda sambamba na uzinduzi wa bunge hilo lililohudhuriwa na viongozi wengine wakuu akiwemo makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hasan, Rais wa Zanzibar Daktari Husen Mwinyi, makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete, makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar mstaafu balozi Seif Ali Idd pamoja na mawaziri Wakuu wastaafu wa Tanzania.